Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora na Mbunge wa Kibakwe, Mhe. George Simbachawene amekerwa na
wananchi wanaoendesha shughuli za kilimo katika milima ya Kibakwe huku akihofia
kama hatua za haraka hazitachukuliwa vyanzo vya maji vitakuwa hatarini
kutoweka.
Mhe. Simbachawene ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza
na wananchi kwa nyakati tofauti kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika
Kijiji cha Lutarawe, Njiapanda na Kikuyu, Jimbo la Kibakwe, Halmashauri ya
Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma ambapo amesema vyanzo hivyo vya maji ni tegemeo
pekee la wakazi wa Jimbo hilo.
Amesema maji yanayotoka katika milima hiyo yana manufaa
makubwa kwa watu wote ilhali mazao yanayolimwa katika milima hiyo ni kwa ajili
ya manufaa watu wachache.
Amesema vyanzo hivyo vya maji ndio vyanzo pekee
vinavyotegemewa lakini kasi ya ukataji miti inazidi kushamiri juu ya milima
hiyo kwa ajili ya kilimo, hali inayotishia maisha ya watu wote kwa ajili ya
maslahi ya watu wachache.
Kufuatia hatua hiyo Mhe. Simbachawene amewataka Madiwani kwa
kushirikiana na viongozi wa vijiji kuzungumza na wanaolima juu ya milima hiyo na kama hawatawaelewa basi sheria
kali zichukuliwe dhidi yao kwani wanahatarisha uhai wa wananchi wa Kibakwe na
taifa kwa ujumla.
"Milima mingi imebaki vipara miti mingi imekatwa kwa
ajili ya kilimo hali inayochangia wakati wa mvua maji kushuka kwa kasi kutoka
milimani na kusababisha uhalibifu wa miundombinu ya barabara, hii sio sawa
kabisa, nawaagiza viongozi chukueni hatua za haraka kwani mnawajua kwa majina
wanaoyafanya hayo," amesisitiza Mhe. Simbachawene.
Kutokana na uharibifu huo, Mhe.Simbachawene amesema tatizo
la maji katika jimbo hilo halitaisha hata kama Serikali itatoa fedha kwa vile
vyanzo vya maji vinazidi kuharibiwa.
Mhe. Simbachawene amesema juhudi anazozifanya za kuwaletea
miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya, shule, barabara pamoja na
umeme itakuwa haina maana kama vyanzo hivyo vitatoweka kwani maji ni uhai.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Ipera, Mhe. Festo Muyuguye
amesema Waziri Simbachawene analitendea haki Jimbo la Kibakwe hususani Kata ya
Ipera katika kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo umeme, ujenzi Kituo cha
Afya, gari la kubebea wagonjwa pamoja ujenzi wa shule za Sekondari.
Hivyo Mhe. Muyuguye ametumia fursa hiyo kuwaomba wananchi wa Kata ya Ipera wasikubali kuyumbishwa na yeyote bali wawalinde Viongozi wao kwa nguvu zote.
0 Maoni