Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini
(TARURA) Mhandisi Victor Seff amewaomba wananchi kutunza na kulinda miundombinu
ya barabara ikiwemo taa za barabarani.
Mhandisi Seff ametoa wito huo wakati wa ukaguzi wa barabara
zilizojengwa na TARURA kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya ‘Ecoroads’ wilayani
Chamwino.
“Serikali imewekeza fedha nyingi kwa kujenga miundombinu hii
hivyo wananchi wanao wajibu wa kusaidia katika utunzaji na kulinda miundombinu
ya barabara ili iweze kudumu kwa muda mrefu.”
Alisema wapo baadhi ya wananchi wanaiba betri za taa za barabarani hivyo ni wajibu wao kuzilinda
na kuzitunza taa hizo kwa manufaa ya
maeneo yao.
Hata hivyo amewataka wananchi kutoa taarifa kwenye ofisi za Wakala
huo mahali popote wanapoona sehemu ya barabara ina changamoto au inahitaji
matengenezo ya haraka ili wafike kutengeneza.
Aidha, Mhandisi Seff alisema kuwa ujenzi wa barabara za
Chamwino umezingatia Usalama wa watumiaji wa aina zote wa barabara hususani
watembea kwa miguu hivyo amewataka wananchi wanaotembea kwa miguu na wale
wanaofanya mazoezi kutumia njia za pembeni za watembea kwa miguu
‘walkways’ ili kuepuka ajali za
barabarani na kujenga afya zao.
Naye, Bi. Rehema Mahajili mkazi wa Chamwino mtaa wa Umoja
amesema wanafurahi kuona barabara zinabadilika ambapo imewasaidia kuboresha
usafiri hususani kuzifikia huduma za afya na kuwaepusha kutembea kwenye vumbi
kwakuwa barabara sasa hivi zimekuwa nzuri.
Barabara za Chamwino zenye urefu wa Km. 6.95 zimejengwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya kuboresha udongo kabla ya kuweka lami juu ijulikanayo kama ‘Ecoroads’ ambapo teknolojia hiyo imetumika kujenga barabara katika wilaya ya Mufindi, Rufiji pamoja na Dodoma mjini.
Na. Catherine Sungura- Dodoma
0 Maoni