Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa ametoa wito kwa taasisi
zote za dini nchini kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutoa mchango
kwenye maendeleo ya taifa.
Mhe. Majaliwa amesema kuwa taasisi za dini zina uwezo mkubwa
wa kutoa huduma imara za kiroho na kugusa maisha ya watu katika jamii na
kuwaletea maendeleo ya kiuchumi na kisiasa.
Ametoa wito huo leo (Ijumaa, Julai 19, 2024) kwenye Kilele
cha Mkutano wa Baraza la Maaskofu wa Makanisa ya Pentekoste Tanzania (CPCT),
uliofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Biblia Miyuji jijini Dodoma.
“Tuna kila sababu ya kuyashukuru Makanisa kwa kuunga mkono
juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuleta maendeleo ya wananchi kwa ujumla,
yamekuwa sehemu ya suluhisho katika changamoto za kijamii kama vile umaskini,
elimu duni, na matatizo ya kiafya,” alisema Mhe. Majaliwa.
“Nitumie fursa hii kusisitiza taasisi za dini kuendelea
kuimarisha ushirikiano na Serikali na kuendelea kuiishi kwa vitendo kaulimbiu
yenu ya Palipo na Umoja, Bwana huamuru baraka! Bwana huamuru baraka, palipo na
Umoja.”
Katika hatua nyingine Mhe. Majaliwa amesema kuwa Serikali
inathamini uwepo na mchango wa taasisi za dini katika kuhubiri amani na utulivu
nchini “Siri ni ya haya yote ni sababu ya uwepo wa dini katika kuhubiri
maadili, mshikamano, upendo uvumilivu na kuwa wamoja, Serikali pekee
tusingeweza.”
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu wa Makanisa
ya Pentekoste Tanzania (CPCT) Dkt. Barnabas Mtokambali amesema kuwa Baraza hilo
kupitia kwa madhehebu wanachama wake litaendelea kushirikiana na Serikali
katika kuendeleza sekta za elimu, na afya nchini kwa kujenga na kuendesha
mahospitali, vituo vya afya, mashule, vyuo vya aina mbalimbali.
“Hili sio tu kwamba linapunguza mzigo mkubwa wa Serikali
katika kuihudumia jamii kubwa ya watanzania katika mahitaji husika, bali pia
linasaidia kupunguza tatizo kubwa la ukosefu wa ajira kwa vijana.”
Ameongeza kuwa CPCT itaendelea kushirikiana na Serikali
katika kuhimiza maadili mema kwa mafundisho ili kupinga wimbi la mmomonyoko wa
maadili linaloukumba ulimwengu mzima.
“Baraza limekuwa mstari wa mbele kupinga vitendo kama ndoa za jinsia moja, ushoga, kutokuwajibika kwa wazazi kutunza familia kunakopelekea kuongezeka kwa Watoto wa mitaani, mila potofu za ukeketaji wanawake, Imani za kishirikina zinazopelekea watu wenye ulemavu wa ualbino kuuawa kwa dhana.”
0 Maoni