Serikali za wilaya zatakiwa kudhibiti shughuli za kibinadamu hifadhini

 

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula (Mb) amezikumbusha Serikali za Wilaya na Vijiji ambavyo vimepakana na Hifadhi za Taifa, Hifadhi za Misitu na Mapori ya akiba wajibu wao katika kushiriki kudhibiti uanzishwaji wa shughuli za kibinadamu karibu na mipaka ya hifadhi hizo.

Mhe. Kitandula ametoa rai hiyo wakati akiongea na wananchi wa kata ya Matemanga Wilayani Tunduru Mkoa wa Ruvuma wakati akiendelea na ziara ya kikazi kwenye maeneo yenye changamoto ya Tembo kwa lengo la kukutana na wananchi kuelezea jitahada zinazofanywa na serikali kudhibiti changamoto ya wanyama wakali na waharibifu.

Akitoa rai hiyo, Mhe. Kitandula alitanabaisha kuwa moja ya sababu zinazochangia kuwepo kwa changamoto ya migogoro kati ya binadamu na wanyama wakali na waharibifu ni shughuli za kibinadamu kwenye hifadhi na kandokando ya mipaka ya hifadhi. Shughuli hizo huharibu ikolojia ya maeneo hayo hivyo kuwafanya wanyama kutoka kwenye maeneo yaliyohifadhiwa na kuvamia mashamba yaliyoanzishwa pembeni ya maeneo hayo.

Aidha, Mhe. Kitandula aliongeza kuwa serikali za vijiji ambazo zinaruhusu wafugaji wenye makundi makubwa ya ng’ombe kuingia katika maeneo yaliyohifadhiwa na kufanya uharibifu wa vyanzo vya maji na mazingira wanayoishi huwafanya wanyama kuingia kwenye maeneo wanayoishi binadamu kwa ajili ya kutafuta maji na chakula kama mahitaji yao ya kila siku.

Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Mhe. Simon Chacha ameishukuru Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuendelea kuweka juhudi mbalimbali za kupambana na wanyama wakali na waharibifu hususani tembo na yeye kama Mwenyekiti wa kamati ya Usalama ya Wilaya atahakikisha yale yote wanayotakiwa kuyafanyia kazi ikiwemo matumizi yenye tija ya Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi wanayafanyia kwa uzito mkubwa.

Na. Anangisye Mwateba- Tunduru Ruvuma


Chapisha Maoni

0 Maoni