TAWA yatoa msaada wa madawati kwa Shule ya Msingi Changarawe

 

MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA imetoa msaada wa madawati 60 yenye thamani ya Shillingi Millioni 5 (5,000,000) kwa Shule ya Msingi Changarawe iliyopo kata ya Mzumbe, Kijiji cha Changarawe wilayani Mvomero Mkoa wa Morogoro.

Akikabidhi madawati hayo kwa niaba ya Kamishna wa TAWA katika hafla ya kukabidhi madawati hayo iliyofanyika Julai 22, 2024 wilayani humo, Kamanda wa Uhifadhi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam Sylvester Mushy alimhakikishia Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Judith Nguli kuwa TAWA itaendelea kushirikiana na wilaya yake kwa kusaidia miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kukabiliana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu.

Aidha, Kamanda Mushy amemshukuru Mkuu huyo wa Wilaya kwa kuitikia wito wa kuhudhuria hafla ya kukabidhiwa madawati hayo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Judith Nguli ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mipango yake ya kuiwezesha Wilaya hiyo, pia ameipongeza TAWA kwa ufadhili walioutoa kwa wanafunzi wa Wilaya yake .

"Nichukue nafasi hii kuishukuru TAWA kwa uwepo wake katika Wilaya ya Mvomero kama wadau wa Uhifadhi, pia tunaishukuru Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mipango yake ya kuiwezesha TAWA kifedha kwasababu imetusaidia sisi wananchi wa Mvomero kupata huduma ya madawati na vilevile kukabiliana na tatizo la wanyamapori wakali na waharibifu," amesema.

Mhe. Judith ameongeza kusema kuwa ufadhili wa madawati 60 uliotolewa na TAWA katika Shule ya  Msingi Changarawe utasaidia kuondoa changamoto ya wanafunzi kukaa chini wakati wa masomo yao.



Chapisha Maoni

0 Maoni