Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa ameitaka Bodi Mpya ya Ushauri ya Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kuwasaidia na kuwashauri watendaji wafanye kazi vizuri ili kuhakikisha anayoyaota Mhe. Rais kwa Watanzania yanatimia.
Mhe. Mchengerwa ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa Bodi ya
Wakala huo ulofanyika jijijni Mbeya.
“Mwenyekiti wa bodi mutakuwa na kazi kubwa ya kuwashauri
watendaji hawa, niwaombe mtusaidie na kutushauri kwani wananchi wanataka
barabara na bajeti ya TARURA imeongezeka kutoka milioni 200 hadi kufika Tilioni
1.3”.
Hata hivyo ameitaka bodi hiyo kuwa wabunifu na kujipanga ili
barabara zinazosimamiwa na TARURA zikamilike pia washirikiane na wataalam
kuhakikisha mchakato wa kuanzishwa kwa hati fungani unakamilika na kuzinduliwa
ili kuwasaidia wakandarasi wazawa.
Aidha, Waziri Mchengerwa ameipongeza TARURA kwa kazi kubwa
walizofanya nchini za ujenzi na matengenezo ya barabara na madaraja licha ya
kusombwa na maji wakati wa mafuriko.
“Nimpongeze Mtendaji Mkuu kwa kazi nzuri anayofanya, pongezi
hizi zishuke hadi kwa watumishi wa chini
kwani matokeo ya kazi nzuri zinaonekana
kwa wananchi.
“Tuna kazi kubwa ya kufanya kwa Taifa letu bidii na
kujitolea inahitajika, tumefanya kazi kubwa na nzuri ila yakaja mafuriko
yakasomba barabara na madaraja, kwa sasa hakikisheni tunajenga upya barabara na
madaraja,“ aliongeza.
Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge Huduma za Jamii Mhe.
Justine Nyamoga alisema kamati yake
itatoa ushirikiano ili kuleta tija kwa wananchi na kusimamia utekelezaji wa
Ilani ya uchaguzi.
Wakati huo huo Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor Seff
alisema bodi hiyo ni ya pili tangu kuanzishwa kwa Wakala huo.
Pia jukumu kubwa la Bodi ya Ushauri ni kumshauru Waziri OR-TAMISEMI kwenye mipango ya kimkakati, namna ya kufikia malengo, upangaji wa vipaumbele, mipango ya bajeti, tathimini na ufuatiliaji wa taarifa mbalimbali za utendaji kazi pamoja na maeneo mengine ya TARURA.
Na. Catherine Sungura- Mbeya
0 Maoni