Bodi ya wadhamini TANAPA yateta na watumishi Serengeti

Bodi ya Wadhamini ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) ikiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi Jenerali (Mst) George Waitara imefanya ziara ya kikazi katika Hifadhi ya Taifa Serengeti.

Ziara hiyo ya siku mbili ya Bodi ya wadhamini ya TANAPA ilitanguliwa na kikao cha watumishi wote wa Hifadhi ya Taifa Serengeti kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano Seronera Serengeti.

Katika kikao hicho Maafisa na Askari wa Jeshi la Uhifadhi walipata fursa ya kuzungumza na Bodi ya Wadhamini na kueleza mafanikio pamoja na changamoto wanazokabiliana nazo katika kutekeleza majukumu ya ulinzi wa Maliasili zote zilizopo hifadhini kikamilifu ikiwa ni pamoja na kuimarisha huduma za utalii na usalama wa wageni wote wanaotembelea hifadhi.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania, George Waitara amewahakilishia maafisa na askari kuwa Bodi ya wadhamini ipo karibu nao wakati wote na kwamba itaendelea kusimamia maslahi na mazingira mazuri ya kazi yanaendelea kuboreshwa ili kuongeza morali na kuleta tija.

“Bodi wakati wote inahakikisha kuwa inaielekeza Menejimenti ya Shirika kuweka vipaumbele katika kuboresha mazingira ya kazi na kutimiza stahiki za watumishi ili waweze kutekeleza majukumu ya kila siku ya kulinda rasilimali za Taifa kwa faida ya watanzania wote” alieleza Jenerali Waitara.

Aidha, Waitara aliwaasa watumishi wote katika Shirika kujikita katika utekelezaji wa majukumu yao kwa mujibu wa viapo walivyoapa na kamwe wasiruhusu watu ambao hawalitakii mema Shirika kuwavuruga kwa namna yoyote ile.

“Mafanikio yaliyopo kwenye Shirika yanapaswa kulindwa na kila mmoja, hivyo jambo la msingi ni kuhakikisha kuwa Maafisa na Askari wa Uhifadhi mnadumisha umoja, mshikamano,nidhamu na kujituma wakati wote ili Shirika liweze kufikia malengo yake  tusiruhusu mtu yoyote kurudisha nyuma jitihada zilizopo kwa sasa ”aliendelea kueleza Jenerali Waitara.

Naye, Kamishna wa Uhifadhi – TANAPA, Musa Nassoro Kuji, alieleza kuwa Hifadhi ya Taifa Serengeti imekuwa ni nguzo muhimu kwa nchi kwani katika mwaka wa fedha uliopita wa 2023/2024, Serikali  kupitia Shirika lilifanikiwa kukusanya Shilingi za Kitanzania Bilioni 410 na kati ya hizo, Hifadhi ya Taifa Serengeti ilichangia kwenye makusanyo hayo kwa asilimia hamsini na nne na kupongeza kazi kubwa na ya kizalendo kwa Taifa letu  inayoendelea kufanywa na Maafisa na Askari katika Hifadhi hiyo ya Serengeti.

“Watumishi wa Hifadhi ya Taifa Serengeti wanachapa kazi usiku na mchana ili kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha kuwa nchi yetu inaendelea kufanya vizuri kwenye sekta ya Uhifadhi na Utalii na hatimaye kupata mapato yatakayoiwezesha Serikali kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili watanzania,” alieleza Kamishna Kuji.

Nao watumishi wa Hifadhi ya Taifa Serengeti wameihakikishia Bodi ya wadhamini kuwa wapo timamu wakati wote katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku kwa kujituma zaidi pamoja na kuhakikisha ulinzi na usalama wa hifadhi na watalii unaendelea kuimarishwa wakati wote.

Bodi ya Wadhamini imehitimisha ziara yake katika Hifadhi ya Taifa Serengeti leo kwa kutembelea uwanja wa mchezo wa gofu uliopo eneo la Fort Ikoma unaoendelea kutengenezwa. Mchezo wa gofu utatumika kama zao jipya la utalii wa michezo katika Hifadhi ya Taifa Serengeti.

Na. Andrew Charles- Serengeti


Chapisha Maoni

0 Maoni