RPC Mutafungwa asimikwa kuwa Mtemi apewa jina la Sangija

 

Wazee wa kata ya Kanyelele wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza wamemsimika Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza Kamishna Msaidizi wa Polisi DCP Wilbrod Mutafungwa kuwa Mtemi wao na kumpa jina la Sangija

Wazee hao wamesema wamefikia uamuzi huo kutokana kuridhishwa na utendaji kazi wa kamanda huyo pamoja na watendaji wengine wa jeshi la polisi katika Mkoa wa Mwanza.

Thomas Shunashu ni Mtendaji wa kata ya Kanyelele amesema kata hiyo yenye wakazi zaidi ya elfu kumi na tano ina vijiji vitano ambapo wakazi wake wameelimika na kuacha kuwapiga wahalifu pindi wanapowakamata.

"Katika kata hii ya Kanyelele wakazi wote wameshaelimishwa na polisi kata hakuna mtu anayempiga mhalifu wakimkamata wanamkabidhi kwa jeshi la polisi na haya ni matokeo ya elimu ambayo polisi kata amekuwa akiitoa mara kwa mara, sasa hivi Kanyelele ipo shwari kabisa sungusungu wapo macho muda wote na wanashirikiana vizuri na askari waliopo hapa.”

Kwa upande wake Diwani wa Kata hiyo ya Kanyelele Daniel Makoye akampongeza Kamanda Mutafungwa kufika katika kijiji cha Kanyelele na kuzungumza na wakazi wake ambao kutokana na utendaji wake wa kazi wakaamua kumsimika kuwa Mtemi wao na kumpa jina la Sangija.

"Kwakweli kamanda Mutafungwa umekuwa kamanda wa mfano katika mkoa huu kwa kuweza kuwafikia wananchi walipo hata mimi leo siamini kama umeweza kufika Kanyelele nikupongeze sana kwa kazi nzuri unayoifanya na wananchi hawa kuamua kukusimika kuwa mtemi wao ni kutokana na utendaji wako wa kazi unaamua kutoka ofisini na kuwatembelea kujua changamoto zao kwa hilo nikupongeze."

Jeshi la polisi mkoa wa Mwanza limekuwa likifanya mikutano ya mara kwa mara na wakazi wake kwa lengo la kufahamu changamoto wanazokutana nazo na kuzitafutia ufumbuzi kwa kuendelea kuimarisha ulinzi na usalama kwa wakazi hao.

Wazee wa Kata ya Kanyelele wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza wakimsimika Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza Kamishna Msaidizi wa Polisi DCP Wilbrod Mutafungwa kuwa Mtemi wao na kumpa jina la Sangija.

Wakazi wa Kata ya Kanyelele wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza wakifuatilia hafla ya kusimikwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza Kamishna Msaidizi wa Polisi DCP Wilbrod Mutafungwa kuwa Mtemi wao na kumpa jina la Sangija.


Shamrashamra za wakazi wa Kata ya Kanyelele wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza katika hafla ya kusimikwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza Kamishna Msaidizi wa Polisi DCP Wilbrod Mutafungwa kuwa Mtemi wao na kumpa jina la Sangija.



Chapisha Maoni

0 Maoni