TARURA Mkoa wa Tabora imepokea fedha za dharura kiasi cha
shilingi milioni 790 kwaajili ya
kurejesha mawasiliano ya miundombinu ambayo yameathiriwa na mvua za Elnino
mkoani humo.
Meneja wa TARURA Mkoa wa Tabora, Mhandisi Lusako Kilembe
amesema kwamba fedha hizo zitatumika kurejesha mawasiliano ya barabara ambazo
zilikatika kutokana na mvua hizo ili wananchi waweze kuendelea na shughuli zao
za kawaida.
“Sasa hivi tumeanza kurejesha mawasiliano ya miundombinu
katika Manispaa ya Tabora, pia katika wilaya nyingine kazi ya kurejesha
mawasiliano ya miundombinu inaenda kuanza hivyo wananchi wataweza kupata huduma
za kijamii na kuendelea na shughuli zao za kiuchumi,”alisema.
Aidha, Mhandisi Kilembe alitaja fedha hizo za dharura
zimepelekwa katika wilaya zote, barabara ya Igunga-Itumba-Simbo milioni 100
(Igunga), milioni 73 barabara ya
Kazaroho-Mpandamlowoka (Kaliua), barabara ya Mwangoye-Senge-Nindo-Mwamala
milioni 92 (Nzega), barabara ya
Kitangili-Mbogwe-Nhele milioni 64.8 (Nzenga TC) barabara ya Usunga-Imalampaka
na Urafiki-Mwanasongezya milioni 57 (Sikonge) na barabara ya Ndeyelwa na
Kakola-Ikomwa na Igombe-Igambilo milioni 275 (Manispaa ya Tabora).
Amesema fedha hizo zitatumika kufukia mashimo kwa kujaza
vifusi, ujenzi wa Kalavati, kunyanyua tuta za barabara, kuweka changarawe,
kurekebisha kingo za maji, ujenzi wa boksi kalavati, kuimarisha kingo za
madaraja pamoja na kuondoa maji kwenye mitaro ya barabara.
Hata hivyo Meneja huyo amewataka wananchi kutunza
miundombinu kwani fedha nyingi zinatumika kujenga barabara hivyo wanapaswa
kulinda miundombinu ili kusitokee watu watakaoharibu kingo za barabara pamoja
na alama zake na endapo itatokea hivyo ni vyema wakatoa taarifa kwenye mamlaka
za serikali.
“Nitoe rai kwa wananchi waweze kulinda miundombinu hii kwakuwa
wapo baadhi ya watu wana tabia ya kukata bomba na vifaa vingine kwenye kingo za
madaraja pamoja na alama za barabarani, watambue kwamba serikali inatumia fedha
nyingi kurejesha miundombinu hiyo na wao kama
watumiaji wa barabara hizo wanapaswa kuzilinda ili ziweze kutumika kwa
muda mrefu," alisema.
TARURA mkoa wa Tabora
unahudumia mtandao wa barabara wenye urefu wa km. 8,404.88 kati ya hizo km.112
za lami, km. 620 barabara za udongo, km. 2007 barabara za changarawe.
Naye, Mtendaji wa kijiji cha Magoweko Bw. Onesmo Halinga
amesema wanaishukuru sana serikali chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan
kwa kuwapatia fedha na hivyo kurejesha mawasiliano ambayo kipindi cha masika
barabara zilikatika.
Amesema mvua hizo zilisababisha gharama za usafiri kupanda ila kwa sasa mawasiliano yamerudi na wanaendelea na shughuli zao za kawaida na pia wanaishukuru TARURA kwa usimamizi wao mzuri kwani sasa hivi barabara zinapitika.
0 Maoni