BAJETI YA 2024-2025: Rais Samia aelekeza kikokotoo kuongezwa

 

Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali imesikia kilio cha wafanyakazi kuhusu kikokotoo na Rais Samia Suluhu Hassan ameelekeza kuongezwa kikokotoo cha malipo ya mkupuo kutoka asilimia 33 ya sasa hadi kufikia asilimia 40.

Hatua hiyo ya kuongeza malipo ya mkupuo kwa kutumia kikokotoo kipya imekuja kufuatia kilio cha wafanyakazi kulalamikia kikokotoo kilichokuwapo cha malipo ya mkupuo ya asilimia 33, kuwa ni kidogo na kinawapunja mafao yao.

Awali mabadiliko hayo ya kikokotoo yalishusha kundi la wafanyakazi waliokuwa wakipokea malipo ya mkupuo wa asilimia 50 mpaka asilimia 33 na kundi waliokuwa wakipokea asilimia 25 walipandishwa mpaka asilimia 33.

Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba amesema, Serikali sikivu inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, imesikia kilio hicho na imekifanyia kazi kwa maslahi mapana ya wastaafu na wanaotarajiwa kustaafu.

“Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameelekeza kuongezwa malipo ya mkupuo kutoka asilimia 33 iliopo sasa hadi asilimia 40,” alisema Dkt. Nchemba jana akiwasilisha Bajeti ya Serikali ya 2024-2025.

Ameongeza kuwa “Hili ndio kundi kubwa la watumishi wanaofanya kazi nzuri sana kwa taifa letu wakiwepo, Walimu, kada ya afya, Polisi, Magereza, Uhamiaji, Zimamoto na makundi mengine yalioko Serikali kuu na Serikali za Mitaa.”

Dkt. Nchemba amesema vilevile, Mheshimiwa Rais ameelekeza kuongezewa zaidi kundi lililokuwa likipokea asilimia 25 hapo awali na kupandishwa kwenda asilimia 33 sasa itakuwa asilimia 35 kuanzia mwaka huu wa fedha.

Watumishi takriban 17 walioathirika na mabadiliko haya watazingatiwa katika mabadiliko haya. Serikali itaendelea kuangalia maslahi ya wastaafu kwa kuzingatia tathmini ya uhai na uendelevu wa mifuko.

Chapisha Maoni

0 Maoni