Jeshi la Uhifadhi lapigwa msasa matumizi ya bomu baridi kukabiliana na wanyama wakali

 

Shirika la Mzinga lenye Makao Makuu yake mjini Morogoro kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI)  wameendesha mafunzo kwa askari kutoka TANAPA, TAWA, TFS na askari wa vijiji (VGS) ili kukabiliana na changamoto ya uvamizi wa Tembo katika makazi ya wananchi na kuleta adha ya mara kwa mara.

Mafunzo hayo yanayoendeshwa kikanda, kwa Kanda ya Kusini yamewahusisha maafisa na askari wa  Uhifadhi kutoka Hifadhi ya Taifa Ruaha na Pori la Akiba la Mpanga- Kipengele ambao ndio kimbilio la wananchi wanapovamiwa na wanyamapori hao yataleta ahueni na kuondoa kero iliyokuwa ikiwasumbua wananchi kwa muda mrefu.

Akielezea mfumo (mechanism) uliotengeneza bomu hilo itakavyoweza kuwakimbiza tembo, Meja Erick Siara kutoka Shirika la mzinga alisema, "Bomu hili lina muunganiko wa vitu vitatu ambavyo ni pilipili iliyomo, sauti ya mlipuko ni kubwa na mwanga. Na kama tunavyojua tembo hapendi mwanga, kelele wala muwasho wa pilipili katika pua zake, hivyo ni matumaini yangu kuwa bomu hili litaleta mapinduzi makubwa."

Mbali na kuleta ufanisi unaokusudiwa wa bomu hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Mhe. Timotheo Mnzava (Mb) wakati wa hafla ya kupokea mabomu hayo May 13, 2024 aliwasihi TAWIRI kuendelea kufanya tafiti mbalimbali ili kuja na njia nyingine mbadala za kukabiliana na tembo, ukizingatia kuwa wanyama hawa kulingana na akili yao wamekuwa wakizoea mbinu fulani kwa haraka zaidi na baadae huendelea kuwa kero tena.

Naye, Mtafiti kutoka TAWIRI - Revocatus Mneney alisema kuwa zoezi la kufukuza tembo ni shirikisho, hivyo ni wajibu wa taasisi za Wizara ya Maliasili na Utalii kushirikiana na wananchi ili kuleta ufanisi na matamanio tarajiwa kwa wananchi husika.

Aidha, Afisa Uhifadhi Mwandamizi - Hera Haima alisema, "Wana matumaini makubwa sana na bomu baridi hilo wakati wa kufukuza tembo hao, kwani kishindo kinachotolewa na mwanga ni mkubwa kitu ambacho temba hakiimili."

Hata hivyo, Mhifadhi Haima  pia aliwataka askari atakaokuwa nao uwandani na wale wote waliopata mafunzo hayo kuzingatia matumizi sahihi ya bomu hilo ili yalete tija iliyokusudiwa na Wizara.

Mafunzo hayo ya matumizi ya mabomu baridi ya kufukuzia wanyamapori wakali na waharibifu yamefanyika leo tarehe 24.05.2024 katika kituo cha Ikoga kilichomo ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha wilayani Mbarali katika mkoa Mbeya, huku ikiwahusisha TANAPA, TAWA, TFS na Askari wa Maliasili Vijijini (VGS).

Na. Jacob Kasiri- Mbarali

Chapisha Maoni

0 Maoni