Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Makonda ameupongeza uongozi
wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwa kuweka malengo makubwa ya kukuza
utalii na kuongeza idadi ya wageni wanaotembelea eneo hilo kwa mwaka ujao 2025.
Mhe. Makonda ameeleza kuwa juhudi zilizowekwa na NCAA za
kutangaza utalii, kuboresha miundombinu ya utalii, kujenga huduma za malazi na
mafunzo kwa watumishi wanaohudumia wageni ziende sambamba na ushirikishwaji wa
wananchi wa mkoa wa Arusha ambao ni wadau muhimu wa kujua vivutio vilivyopo ili
wanapokutana na wageni katika maeneo mbalimbali wawe na uwezo kuelezea fursa za
utalii zilizoko mkoa wa Arusha.
“Mikakati mliyonayo ni ya kupongezwa, mwaka uliopita
mlifikisha wageni takribani 752,000, naamini mwaka huu mtavuka zaidi, mikakati
mliyoiweka ni tafsiri ya vitendo na maono ya Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan
kuitangaza nchi yetu kupitia filamu ya Tanzania the Royal tour , sasa naomba
utekelezaji wa mipango hii kwa kila hatua kuwe na ushirikishwaji na elimu kwa
wananchi wa Mkoa wa Arusha, Serikali ya Mkoa na Wilaya ya Karatu,” aliongeza
Mhe. Makonda.
Akitoa taarifa ya mendeleo ya utalii katika eneo la hifadhi
ya Ngorongoro, Kaimu Kamishna wa Uhifadhi NCAA Vicktoria Shayo ameeleza kuwa
idadi ya wageni imeendelea kuongezeka ambapo kati ya Julai 2023 hadi aprili,
2024 jumla ya wageni 780,281 wameshatembelea eneo la hifadhi Ngorongoro.
Kamishna Shayo amebainisha kuwa kwa sasa Serikali kupitia
NCAA inaendelea kuboresha shughuli za uhifadhi na kuboresha maendeleo ya
wananchi ikiwemo kuboresha huduma bora zaidi za kijamii nje ya hifadhi hasa
katika Kijiji cha Msomera, Kitwai na Saunyi ambapo Serikali inaendelea kujenga
nyumba za makazi na miundombinu mingine ya kijamii kwa ajili ya wananchi
wanaoendelea kujiandikisha kuhama kwa hiari.
Katika hatua nyingine, Mhe. Makonda ametembelea mradi wa
ujenzi wa jengo la makao Makuu ya NCAA Karatu Mkoani Arusha ambapo ujenzi huo
ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa kupunguza shughuli za binadamu ndani ya
Hifadhi ili kuboresha uhifadhi na kuboresha maisha ya wananchi wa Ngorongoro na
kuwajengea miundombinu bora ya kijamii nje ya Hifadhi.
Akitoa taarifa za ujenzi wa jengo hilo Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa uhifadhi huduma za Uhandisi NCAA Mhandisi Daniel Chegere amesema ujenzi huo katika awamu ya kwanza unahusisha Jengo la ofisi za makao makuu na nyumba tatu za viongozi wakuu wa shirika ambapo ujenzi huo umefikia asilimia 80 na unatarajiwa kukamilika mwezi Julai mwaka huu.
0 Maoni