NAIBU Waziri wa Madini, Mheshimiwa Dkt. Steven Kiruswa (Mb.)
ametoa maelekezo matano kwa Tume na wadau wa Sekta ya Madini nchini.
Akifunga Jukwaa la Tatu la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa
Watanzania katika Sekta ya Madini leo Mei 24, 2024 kwenye Ukumbi wa AICC jijini
Arusha, Dkt. Kiruswa ameagiza watanzania kujengewa uwezo ili kuendana na soko
la ajira katika sekta ya viwanda.
Amesema kuwa, Tanzania imefungua milango ya uwekezaji katika
sekta hiyo ikiwemo kuendeleza ushirikiano na wadau wa madini ili kufanikisha
utekelezaji wa mikakati ya Vision 2030 ya Madini ni Maisha na Utajiri hivyo
ni muhimu viwanda vinavyojengwa kwenye migodi viende sambamba
na kuwapa ujuzi Watanzania.
“Ujenzi wa viwanda kwenye migodi, vinahitaji ujuzi sio
kuanzisha tu, nitoe wito uanzishwaji wa viwanda uende sambamba na watanzania
kujengewa uwezo,”amesema Dkt. Kiruswa
Agizo la pili amelitoa kwa wawekezaji wa migodi ni kutoa
udhamini kwa mafunzo yanayofanyika
nje ya nchi kwa watumishi wao ili
kuwajengea uwezo.
Pia, Dkt. Kiruswa ameagiza vyuo kufungamanishwa na
wawekezaji wa viwanda ikiwemo kuandaa Mitaala ili kuendana na mahitaji ya soko
husika.
Dkt. Kiruswa pia ameagiza kuanzishwa kwa program maalum za
kubadilishana uzoefu na mataifa mengine ‘Exchange Program’ ili kuwajengea uwezo
wataalam wa ndani.
“Kuna umuhimu kwa wenye viwanda kutoa fursa kwa vijana wa
vyuo kufanya mafunzo kwa vitendo kwenye viwanda vyao ili wapate ujuzi,” amesisitiza
Mheshimiwa Dkt. Kiruswa.
Aidha, amesema kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuvutia
uwekezaji zaidi hususan katika sekta ya viwanda vya bidhaa za migodini.
Pia, amesema kuwa,
Jukwaa hilo la Ushirikishwaji wa Watanzania lenye kauli mbiu ‘Uwekezaji wa Viwanda vya
Uzalishaji wa Bidhaa za Migodini kwa Maendeleo Endelevu’ ni muhimu kwa wadau wa
Sekta ya Madini kulitumia kama njia ya kutafuta ufumbuzi wa changamoto
zinazowakabili katika utekelezaji wa miradi wanayoisimamia ili kuchochea
uwekezaji.
“Ni matumaini yangu
kuwa kutakuwa na mabadiliko makubwa katika utekelezaji wa suala la ushirikishwaji
wa watanzania kwa wamiliki wa leseni na watoa huduma katika Sekta ya Madini
nchini,”amesema Dkt. Kiruswa.
Awali, akizungumza Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini,
Mhandisi Yahya Samamba amesema kuwa jumla ya mada saba zimewasilishwa katika
jukwaa hilo lililoanza rasmi Mei 22, 2024 ambapo siku ya kwanza ziliwasilishwa
mada mbili, siku ya pili zikawasilishwa mada sita na leo imewasilishwa mada
moja.
“Mada zote lengo ni uchechemuzi wa kuanzishwa viwanda hapa
nchini na bidhaa zote zinazohitajika migodini zipatikane hapa hapa nchini,
Tunaposema kuna ongezeko la watanzania kupata fursa katika Sekta ya Madini
ambalo kwa sasa limefikia asilimia 84 na miaka michache ijayo tutafikia
asilimia 100 lakini ni fursa zipi tunazozifikia?,” amehoji na kuongeza,
“Changamoto kubwa malighafi bado zinatoka nje ya nchi, fursa
iliyopo sasa ni kujenga viwanda hapa hapa nchini, teknolojia za kisasa na
bidhaa zinazotumika kwa wingi migodini zitoke hapa hapa nchini, serikali, watu
binafsi tunawajibika kushirikiana ili kutimiza ajenda ya VISION 2030.
“Tunahitaji kuweka nguvu kubwa katika ‘Local Content na CSR
ili watanzania wengi zaidi waweze kunufaika na Sekta ya Madini,”amesisitiza
Mhandisi Samamba.
Katika kongamano hilo, wadau mbali mbali wa Sekta ya Madini wamepewa tuzo na vyeti kutoka Tume ya Madini lengo ni kutambua mchango wao katika sekta hiyo.
0 Maoni