Dkt. Abbas aipongeza TANAPA kwa kusimamia vyema uhifadhi na utalii

 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas, ametembelea Makao Makuu ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa ajili ya kuongea na Menejimenti ya Makao Makuu na Kanda ya Kaskazini.

Katika kikao chake jana na Menejimenti, Dkt. Abbas aliwapongeza viongozi wa Shirika kwa kuendelea kusimamia vyema shughuli za Uhifadhi na Utalii katika maeneo yote ya Hifadhi za Taifa hapa nchini.

Aliwaeleza wahifadhi kuwa, mbali na changamoto wanazokabiliana nazo bado wanayo nafasi ya kuweka mikakati ya kutatua changamoto hizo ili kuziwezesha Hifadhi za Taifa kuwa maeneo bora zaidi ya kutembelewa na watalii wa ndani na nje ya nchi.

Aidha, ameipongeza TANAPA kwa jitihada inazoendelea nazo za kutangaza vivutio vilivyopo pamoja na kuwapokea watalii na kuwapa huduma zinazokidhi viwango.

“Katika idadi ya watalii waliotembelea nchini, tunatambua kuwa mchango wa TANAPA ni mkubwa katika kuifikia idadi hiyo, Hongereni sana!” - alieleza Dkt. Abbas.

Pia, Dkt. Abbas aliongeza kuwa tarehe 02.05.2024 alitembelea Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro kama sehemu ya mwendelezo wa maadhimisho ya miaka miwili ya filamu maarufu ya “Tanzania: The Royal Tour” na kupokea taarifa ya utendaji kazi ya Hifadhi hiyo.

Aliongeza kuwa zipo baadhi ya changamoto ambazo Kamishna wa Uhifadhi na timu yake ni lazima kuweka mikakati ya kuhakikisha kuwa changamoto zilizopo katika Mlima Kilimanjaro zinapatiwa ufumbuzi wa haraka na wa kudumu ili kuongeza kiwango cha watalii kuridhika na huduma (customer satisfaction) na pia watalii hao waendelee kuwa mabalozi wazuri wa vivutio vilivyopo hapa nchini.

Dkt. Abbas alisisitiza kwa Menejimenti ya TANAPA kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii imejijengea heshima kubwa ndani ya Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni vema heshima hiyo ikalindwa kwa kufanya kazi kwa bidii, uzalendo, uadilifu, kujituma na ubunifu wa hali ya juu.

“Wakati huu ni kipindi ambacho kila mtumishi anapaswa kuweka juhudi katika kutoa ushauri wa kibunifu ili kutatua changamoto zilizopo na pia kuboresha mazingira ya Hifadhi za Taifa” - aliongeza Dkt. Abbas.

Na. Andrew Charles - Arusha

Chapisha Maoni

0 Maoni