Maji ya Ziwa Victoria yaongezeka na kuathiri kaya kadhaa

 

Maji yameogezeka katika Ziwa Victoria na kusababisha athari ambapo baadhi ya kaya Kisiwani Rukuba zimelazimika kuhifadhiwa kwenye kituo cha afya.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge wa Musoma Vijijini Prof. Sospeter Muhongo imesema mvua zinaendelea kunyesha, na maji Ziwa Victoria yanaendelea kuongezeka.

“Siku ya leo tarehe 04/05/2024 siyo nzuri Kisiwani Rukuba, Kaya ya Etaro kwani kaya tano (5) hazina makazi zimehifadhiwa kwenye Kituo cha Afya cha hapo Kisiwani,” imesema taarifa hiyo.

Imeelezwa kwamba maji yanaendelea kuongezeka, na makazi ya kaya nyingine thelathini na mbili (32) yako hatarini.

Kisiwani Rukuba, Kata ya Etaro waathitika wamesema "maji yamewafuata" kwa takribani mita 30-40 hadi kwenye makazi yao.

Kwa upande wao waathirika wa Mji wa Musoma wanaoishi karibu na ufukwe wa Ziwa Victoria wanasema "maji yamewafuata kwa takribani mita 5" hadi kwenye makazi yao.

Mbunge Prof. Muhongo amewasiliana na wataalamu walioko kwenye ya Bonde la Ziwa Victoria Mwanza na kuelezwa maji yameongezeka kwa kiasi cha wastani wa kina cha mita 1.65

Wananchi wanaoishi karibu na ufukwe wa Ziwa Victoria wametakiwa kufuata ushauri watakaopewa na viongozi mbalimbali, kwa ajili ya kuepuka mafuriko au ongezeko la maji ndani ya Ziwa Victoria.

Vilevile, wananchi wanahimizwa kufuatilia utabiri wa hali ya hewa unaotolewa kila siku na wataalamu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa wa (TMA).

“Ziwa Victoria lenye kawaida ya ujazo wa maji wa takribani kilomita za ujazo 2,424 (2,424 cubic kilometres), kwa sasa maji yaongezeka sana! Tuchukue tahadhari kubwa!”, imemalizia taarifa hiyo.

Chapisha Maoni

0 Maoni