Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameshiriki mazoezi ya pamoja ya
kampeni ya kitaifa inayoratibiwa na Wizara ya Afya ya kuhamasisha ufanyaji wa
mazoezi kwa watanzania ili kujiepusha na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Mheshimiwa Majaliwa amesema hatua hiyo pia ni kuunga mkono
wito wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu
Hassan wa kufanya mazoezi ili kujikinga na magonjwa hayo.
Ameyasema hayo leo (Jumamosi Mei 4, 2024) aliposhiriki katika
kampeni ya ufanyaji mazoezi pamoja na matembezi ya kilomita 10 yaliyoanzia
katika fukwe za Coco kupitia daraja la Tanzanite hadi Ocean Road jijini Dar es
Salaam.
"Mnakumbuka programu hii iliyoanzishwa na Rais wetu
Dkt. Samia Suluhu Hassan na yeye mwenyewe kushiriki na kuwahamasisha watanzania
kushiriki mazoezi mbalimbali, katika kipindi cha miaka mitatu ya Dkt. Samia
moja ya mambo ya kujivunia ni mafanikio katika sekta ya michezo."
Kadhalika Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa Viongozi wa Manispaa
ya Kinondoni kufanya maboresho zaidi katika eneo la fukwe za Coco ili liwe safi
na livutie watu wa rika mbalimbali.
"Nawapongeza jeshi la polisi kwa kazi nzuri ulinzi
katika eneo hili, Nitoe wito kwenu kuendelea kuimarisha ulinzi ili eneo hili
liwe salama kwa watu wa rika na jinsia zote."
Awali, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amemshukuru Waziri Mkuu
kwa kukubali kushiriki katika mazoezi hayo huku akitoa taarifa ya ongezeko la
magonjwa 10 yasiyo ya kuambukiza jambo lililofanya Wizara hiyo kuleta ombi la
kuanzishq utaratibu wa mazoezi kila jumamosi.
"Mwaka 2022 kati ya magonjwa 10 yanayowasumbua
watanzania moja lililojitokeza ni shinikizo la juu la damu bajeti ya mwaka
2022/2023 likaongezeka na kisukari katika mahlgongwa 10 yanayowasumbua
watanzania. Wajibu wa Wizara ya Afya ni kuwakinga Watanzania wasipate
magonjwa."
Kwa Upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albart Chalamila amesema kama Mkoa watajipanga kuhakikisha utaratibu huo wa mazoezi utakuwa endelevu kwa kishirikiana na kamati ya Ulinzi na usalama pamoja na wadau mbalimbali wa michezo.
0 Maoni