Watendaji Kata watakiwa kushirikiana na Polisi Kata kukomesha uhalifu

 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Naibu Kamishina wa Polisi (DCP) Wilbrod Mutafungwa amewataka Watendaji wa Kata kushirikiana na Polisi Kata kwenye maeneo yao ili kuzuia uhalifu katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.

Kamanda Mutafungwa ametoa kauli hiyo Wilayani Kwimba wakati akizungumza na watendaji wa kata na vijiji ambao ni walinzi wa amani katika maeneo yao na kuwataka kushirikiana na Polisi Kata kutoa elimu kwa wananchi juu ya kuzuia uhalifu.

"Nimekuja kuwaomba watendaji wa kata mtusaidie kuelimisha wananchi kwa kushirikiana na Wakaguzi Kata kuhusu mambo ya kujichukulia Sheria mkononi ambayo yamesababisha mauaji katika maeneo yenu, alisema Kamanda Mutafungwa na kuongeza, “Tunatamani kuona tunafanikiwa zaidi kuzuia uhalifu kuliko kupambana na uhalifu kwa sababu wote hapa mnaelewa namna ambavyo ni gharama kubwa kupambana na uhalifu na jinsi ambavyo ni gharama nafuu kuuzuia uhalifu."

Nao baadhi ya Watendaji wa Kata wa Wilaya ya Kwimba wameliashukuru Jeshi la Polisi kwa elimu waliyoipata na kuahidi kuongeza ushirikiano zaidi kwa Jeshi hilo ili kidhibiti uhalifu katika maeneo yao.

"Tunashukuru na tunapongeza ujio wa Kamanda Mutafungwa umetusaidia kupitia elimu na ushauri tunaenda kushirikiana na Polisi Kata katika vikao vya Vijiji na WDC, katika suala la ulinzi na amani ngazi ya Kata," amesema Mtendaji wa Kata ya Nyambiti Felister Mazinzi.




Chapisha Maoni

0 Maoni