Katika kuhakikisha usalama wa maisha ya watu wilayani Rufiji, Mamlaka ya Usimamizi wa
Wanyamapori Tanzania - TAWA imefanya msako wa mamba wanaotajwa kutishia maisha ya watu kutokana
na kusogea karibu na makazi ya watu kufuatia kusafirishwa na mikondo ya maji
yaliyosababishwa na mafuriko.
Afisa habari wa TAWA Beatus Maganja akizungumza na waandishi
wa habari katika mji mdogo wa utete wilayani Rufiji leo Aprili 18, 2024 amesema
TAWA inaendelea na msako wa mamba tishio kwa maisha ya watu wilayani humo lengo
likiwa ni kulinda usalama wa wananchi wa
wilaya hiyo.
" Ni wajibu wetu kuimarisha ulinzi ili yasitokee maafa
ya binadamu kupotea kutokana na kuliwa
na mamba wakati sisi tuko hapa,"
amesema Afisa habari huyo.
"Na ndiyo maana tumekuja hapa kuhakikisha tunawasaka
mamba wote ambao ni tishio kwa maisha ya binadamu.
Aidha, Maganja amesisitiza kuwa Sheria ya Uhifadhi wa
Wanyamapori Sura ya Na. 283 inaelekeza kuwadhibiti wanyamapori wakali na
waharibifu endapo itaonekana wana hatarisha maisha ya binadamu, hivyo chochote
wanachokifanya ni kwa mujibu wa sheria lengo likiwa ni kulinda uhai wa
binadamu.
Hata hivyo ametoa wito kwa wananchi wa wilaya hiyo
kuzingatia elimu wanayoendelea kupewa na Maofisa uelimishaji kutoka TAWA ili
kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza kwa kushambuliwa na mamba.
Naye Afisa Mhifadhi wa TAWA George Boniface amesema kutokana
na mvua zinazoendelea kunyesha mamba wengi wamesafirishwa na maji kutoka
Hifadhi ya Taifa ya Mwalimu Nyerere na Hifadhi ya Selous na kufika katika maeneo
ya makazi ya watu katika mji wa utete na viunga vyake wilayani Rufiji kiasi cha
kutishia maisha ya binadamu.
Amesema zoezi linaloendelea eneo hilo ni kuwasaka mamba wote
ambao ni tishio kwa kutega mitego na kwa kutumia boti kwa usaidizi wa wenyeji
na wavuvi.
Vilevile, Hamis Moshi Ipombo ambaye ni mzaliwa na mkazi wa
utete Rufiji anayejihusisha na shughuli za uvuvi amesema katika mto Lugongwe
uliopo eneo la utete kumekuwepo na mamba
mkali anayetishia maisha wakazi wa eneo hilo kwa kukimbiza mitumbwi
wawapo katika shughuli zao, mamba anayetajwa kusakwa na Maofisa wa TAWA.
Hata hivyo ameishukuru Serikali kupitia TAWA kwa kuwapata elimu ya kuepuka madhara yatokanayo na wanyamapori wakali na waharibifu hususani mamba huku akikiri kuwa elimu hiyo imewasaidia kuendelea na shughuli zao za kiuchumi huku wakiwa salama.
0 Maoni