Serikali kupitia wizara ya Maliasili na utalii imezitaka
Taasisi zilizopo chini ya Wizara hiyo kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya
Mvomero katika kutatua changamoto ya tembo ambao wanasababisha madhara kwa
wananchi.
Akizungumza jana mbele ya mamia ya Wakazi wa Vijiji vya
Mangae, Doma na Mkata Wilayani Mvomero, wakati wa Operesheni ya kuyarudisha
makundi ya Tembo Hifadhi ya Taifa ya
Mikumi, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe.Dunstan Kitandula (Mb),amesema
kwa kutumia helikopta makundi yenye
jumla ya Tembo 45 waliokuwa kwenye maeneo ya makazi ya wananchi yamerejeshwa hifadhini
katika zoezi linaloendelea kwa siku ya
kesho.
Mhe, Kitandula ameeleza
zoezi la kuwarejesha tembo
hifadhini ni jitihada za makusudi zilizofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe.Rais Dkt Samia
Suluhu Hassan katika kuwahakikishia
usalama wananchi na uhifadhi endelevu
nchini.
"Zoezi hili la kutumia Helikopta limetumia gharama
kubwa, lakini licha ya ukubwa wa gharama hizi Serikali imejipanga kupunguza
kero kwa wananchi wa maeneo haya ambao kadhia za wanyama hawa zimekuwa
zikihatarisha usalama na mali zao," alisema Mhe.Kitandula.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Bi, Judith Nguli
akimuwakilisha mkuu wa Mkoa wa Morogoro, ameipongeza Serikali
kupitia Wizara ya Maliasi na Utalii kuwezesha zoezi la kuwaswaga Tembo
kwa kutumia Helikopta kwani changamoto
ya Tembo ni ya muda mrefu kwa wananchi.
kwa upande wake Mbunge
wa Mvomero, Mhe.Said Hussein Said amesema uwezeshaji wa zoezi hilo ni faraja kwa wananchi
kwani tembo wamekua wakileta
uharibifu mkubwa wa mali na kuatarisha
usalama wa Wananchi ambapo ameiomba Serikali
kuendelea kuwasaidia
kuepukana na changamoto hiyo.
"Naishukuru Serikali kusikia kilio cha wananchi na
kuchukua hatua baada ya kuleta mapendekezo bungeni na kwa Waziri wa Maliasili
na Utalii."
Akielezea vifaa vya kujikinga na tembo vilivyokabidhiwa na
Wizara kwa wananchi, Mkurugenzi wa Taasisi ya Wanyamapori Tanzania (TAWIRI)
Dkt, Eblate Ernest Mjingo amesema Taasisi hiyo imeendelea kubuni mbinu mbadala
za kutatua changamoto za migongano za kati ya binadamu na Wanyamapori nchini
hususani tembo.
"Tafiti zimesaidia matumizi ya teknolojia katika kutatua
migongano hiyo ikiwa ni pamoja na teknojia ya helkopta na mikanda ya visukuma
mawimbi (GPS Coller)."
Uzinduzi rasmi wa Operesheni
hiyo umefanyika katika Kijiji cha
Maenga Wilaya ya Mvomero na kuwajumuisha
Viongozi wa Chama na Serikali na Viongozi wa kijamii wa Wilaya hiyo.
0 Maoni