Wanafunzi wa kike wapewa baiskeli kuwaepusha na vishawishi

 

Diwani wa kata ya Bujora wilayani Magu, Mwanza Bunyanya John, ametoa msaada wa baiskeli 54 kwa wanafunzi wa kike katika shule ya Sekondari Lumve ili kuwapunguzia adha ya kutembea umbali mrefu kwenda shule.

Akikabidhi baiskeli hizo diwani huyo amesema wanafunzi hao wamekuwa wakipata changamoto mbalimbali zikiwemo za kuvamiwa na wanayama wakali pindi wanapoenda shule huku wengine wakikatisha masomo hivyo baiskeli hizo zitasaidia kuwaondolea changamoto hizo.

“Baiskeli mlizopata leo naomba mzitumie vizuri katika kurahisisha usafiri wa kutoka nyumbani kuja shule ili muweze kuongeza ufaulu maana njiani mlikuwa mnapata chanagmoto nyingi kama kuvamiwa na wanyama wakali, wengine hupata vishawishi na kuishia kukatisha masomo wengine kufanyiwa vitendo vya ukatili, sasa mkazitumie vizuri baiskeli hizi.”

Kwa upande wao wanafunzi Hellen Mmasi na Esther John wameshukuru kupata msaada wa baiskeli hizo na kuahidi kufanya vizuro katika masomo yao.

“Baiskeli hizi zitatusaidia kwa kiasi kikubwa kuepuka changamoto kwani tutawahi shuleni na kufaulu kwa kufanya vyema kwenye masomo yetu kwani tutawahi shule na kupata muda mzuri wa kujisomea,” wamesema wanafunzi hao.

Mdau wa maendeleo aliyeshirikiana na Diwani wa kata hiyo ya Bujora Jefta Kishosha akatoa wito kwa wazazi kuwa mstari wa mbele kuwasaidia watoto wao katika utunzaji wa baiskeli hizo na kuacha kuzitumia kwa matumizi tofauti na yaliyokusudiwa ikiwemo na kubeba mizigo na maji.



Chapisha Maoni

0 Maoni