Serikali ya Tanzania inaandaa andiko la kitaalam la
kuwasilisha Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO)
kuhusu suala la kuweka tabaka gumu la miundombinu ya barabara katika Hifadhi ya
Taifa ya Serengeti, ili kuepuka gharama kubwa za matengenezo ya miundombinu.
Hayo yameelezwa leo Jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Idara ya
Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Mobhare Matinyi, wakati
akiongea na waandishi wa habari kuhusu athari la mvua za El Nino katika Hifadhi
za Taifa za Tanzania ikiwamo ya Serengeti.
“TANAPA na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
zinaandaa andiko la kitaalam la UNESCO kuhusiana na suala la kuweka tabaka gumu
kwani Serengeti imo katika Orodha ya Urithi wa Dunia inayosimamiwa na Kamati ya
Urithi wa Dunia ya UNESCO,” amesema Bw. Matinyi na kuongeza, “ Njia ya kutumia
andiko la kitaalam ndiyo iliyotumiwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la
Ngorongoro (NCAA) ambapo sasa imepata kibali cha kujenga barabara yenye tabaka
gumu.”
Amesema kwamba Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, ambayo pia
imeathirika na El Nino, ni hifadhi ya tatu kwa ukubwa nchini yenye kilomita za
mraba 14,763. Hifadhi kubwa zaidi nchini ni Nyerere ikiwa na kilomita za mraba
30,893 ikifuatiwa na Ruaha yenye kilomita za mraba 19,822 lakini Serengeti
ndiyo hifadhi ya kwanza nchini kwa kuingiza watalii wengi zaidi.
Bw. Matinyi ameeleza kuna barabara kuu nne zenye changamoto
zaidi kutokana na upitaji wa magari makubwa ya abiria na mizigo yanayokwenda
mikoa ya jirani ya Mara, Arusha, Manyara, Mwanza, Shinyanga na Simiyu ambazo
TANAPA ndizo inazozilenga katika mkakati wake wa mbinu mbadala ya tabaka gumu
iwapo itakubalika.
Bw. Matinyi amesema kuwa TANAPA inatarajia kwamba utatuzi wa
kudumu utapatikana katika barabara kuu zinazoihudumia Serengeti na hivyo
kuongeza idadi ya watalii nchini kwa kiasi kikubwa kufuatia matunda ya filamu
ya Royal Tour.
Itakumbukwa kwamba tangu mwezi Oktoba 2023, nchi yetu ilianza
kupata mvua kubwa za El Nino ambazo hadi sasa bado zinaendelea katika baadhi ya
maeneo nchini. Moja ya athari za mvua hizo ni uharibifu wa miundombinu, ikiwemo
barabara za kwenye hifadhi za taifa zilizo chini ya Shirika la Hifadhi za Taifa
(TANAPA) ikiwemo Serengeti, amesema Matinyi.
Pamoja na mambo mengine Bw. Matinyi ametangaza mafanikio ya
ongezeko la watalii nchini kwa kusema licha ya makadirio ya idadi ya watalii
kwa hifadhi zote za TANAPA kwa mwaka 2023/24 kuwa 1,387,987 lakini mpaka
kufikia Februari 2024 (miezi nane tu kuanzia Julai 2023), jumla ya watalii
1,451,176 wameshaingia huku Serengeti ikiwa na wengi zaidi.
0 Maoni