SERIKALI imekamilisha mchakato wa kufanya tathmini ya malipo ya kifuta jasho kwa wananchi 27 wa wilaya ya Nkasi Mkoani Rukwa ambao mazao yao yaliathiriwa na wanyamapori wakali na waharibifu katika kipindi cha mwaka 2022 mpaka 2024.
Kauli hiyo imetolewa Desemba 22, 2024 na Afisa Wanyamapori
Wilaya ya Nkasi Bw. Anorld Ngagashi akiongea na wananchi wakati wa ziara ya
mafunzo ya mbinu za kukabaliana na wanyamapori wakali na waharibifu hususani
tembo, ziara iliyofanywa na TAWA wilayani humo.
"Kwa sasa wananchi wa wilaya ya Nkasi suala la
kifuta jasho lipo asilimia 98, kuna wananchi 27 wanakwenda kulipwa hivi
karibuni shilingi milioni kumi na saba laki saba na elfu hamsini (17,
750,000/=),” amesema Anorld Ngagashi.
Anorld amesema mpaka sasa wananchi watatu kutoka Kata ya
Kabwe (2) na Wampembe (1) wameshalipwa jumla ya shilingi milioni tatu
(3,000,000/=) malipo yaliyofanyika Desemba 20, 2024 na kusisitiza kuwa wananchi
24 waliosalia malipo yao yatakamilika muda wowote kuanzia sasa.
Aidha, Afisa huyo amepongeza ushirikiano mkubwa
wanaoupata kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA kupitia
Pori la Akiba Lwafi katika kukabaliana na changamoto ya wanyamapori wakali na
waharibifu wilayani humo.
"Tunaishukuru Serikali hii ya Rais Samia pamoja na
uongozi wa TAWA kwakweli tumeshirikiana 100%, kwahiyo Kati ya Mikoa yote mfano
wa kuigwa ni Pori la Akiba Lwafi kwani wameonesha ushirikiano mkubwa
kuhakikisha gurudumu hili la kupambana na wanyamapori wakali na waharibifu
tunalisukuma wote Kwa pamoja," amesisitiza Ngagashi.
Kwa upande wake Afisa Habari wa TAWA Beatus Maganja
amesema licha ya matumizi ya teknolojia ikiwemo matumizi ya ndege nyuki TAWA
imewekeza nguvu katika kuwapa elimu wananchi wanaoishi pembezoni mwa Hifadhi
zilizo chini ya usimamizi wa Taasisi hiyo ili wapate uelewa wa namna ya
kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu.
Aidha, amesisitiza kuwa mbali ya changamoto ya
miundombinu kwa vijiji hasa pale Askari wanapolazimika kuitumia kuvuka ili
kuwafukuza wanyamapori waliovamia makazi ya watu, TAWA itahakikisha inafanya
kila linalowezekana kuwafikia wananchi.
"Iwe jua iwe mvua TAWA tutapambana kuhakikisha
tunaokoa maisha ya wananchi," amesisitiza Maganja.
Wananchi wa Nkasi wamepongeza jitihada zinazofanywa na
Serikali kupitia TAWA katika kuhakikisha wanatoa elimu ya mbinu za kukabiliana
na wanyamapori wakali na waharibifu hususani tembo Jambo ambalo wanakiri kuwa
na msaada mkubwa katika kuokoa maisha ya wananchi hao.
0 Maoni