Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini ikiwemo Wilaya ya Magu.
Amesema hayo leo Desemba 23, 2024 wilayani Magu mkoani
Mwanza katika Mkutano Mkuu Maalum ambapo taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya
Uchaguzi Mkuu Jimbo la Magu kwa mwaka 2020 hadi 2024 iliwasilishwa.
“Mhe. Rais amefanya kazi kubwa ya kupigiwa mfano na
anastahili pongezi, nataka
niwaambieni kuna watu wengine
wanaumia tukimpongeza Rais Samia, lakini wajue hatutoi pongezi hizi peke yetu
hata huko duniani kwa mfano Benki ya
Dunia na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wanampongeza kwa ukuaji
wa uchumi wa nchi yetu kwa asilimia 5.1,” amesema Dkt. Biteko.
Amesema pia kuwa Rais Samia ana nia njema na anataka
kuona Watanzania wanapata maendeleo.
Ameongeza kuwa maendeleo katika Jimbo la Magu hayakuja
kwa bahati mbaya isipokuwa kwa mipango na hivyo anawapongeza wanachama wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Magu kwa tamko la pongezi kwa Rais Samia kwa
kuwapa fedha kiasi cha shilingi 143.9 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi
mbalimbali.
Ametaja baadhi ya miradi iliyotekelezwa na Serikali “
Barabara za lami zimeunganisha mikoa yote nchi nzima, tuna ndege za abiria na
mizigo, tumejenga shule nyingi na sasa tunajenga shule za kata maeneo
mbalimbali nchini. Maendeleo yanaonekana kwa macho na sisi ni kazi yetu kusema haya kwa wivu mkubwa.”
Kuhusu umeme Dkt. Biteko amesema katika kijiji kimoja
pekee ambacho hakina umeme, Serikali imetenga fedha kiasi cha shilingi milioni
600 kwa ajili ya kupeleka umeme huku mipango ya kupeleka umeme katika kisiwa
ikiendelea.
Aidha, amempongeza Mbunge wa Jimbo la Magu, Mhe. Kiswaga kwa
usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo.
Dkt. Biteko amesema “CCM ni chama kiongozi hivyo wanaCCM
tembeeni kifua mbele hubirini yanayofanywa na chama chenu waonesheni watu maendeleo
yaliyotokea msiwapuuze.”
Pamoja na hayo amempongeza Mhe. Kiswaga kwa kusimamia
miradi ya maendeleo huku akiwaasa wanachama wa CCM kushirikiana na viongozi kwa
ngazi zote ili kuendelea kuimarisha chama huku akiwapongeza kwa mafanikio
makubwa yaliyopatikana katika Jimbo lao.
Mbunge wa Jimbo la Magu, Mhe. Boniventura Kiswaga wakati
akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi Mkuu Jimbo la Magu kwa
mwaka 2020 hadi 2024 amesema Serikali ya Rais Samia imeendelea kuwapa fedha kwa
ajili ya miradi mbalimbali ikiwemo shilingi
bilioni 78 kwa ajili ya ujenzi wa barabara na madaraja.
Amebainisha kuwa Serikali kupitia Wakala wa Barabara
Tanzania (TANROADS) wametoa fedha kiasi
cha shilingi bilioni 48 kwa ajili ya kujenga daraja la Simiyu.
“Kwenye sekta ya maji tumepokea shilingi bilioni 12 kwa
ajili ya kujenga tanki lenye lita za ujazo milioni 5 litakalohudumia kata 14,”
amesema Mhe. Kiswaga.
Amesema Rais Samia katika bajeti ya mwaka huu ametenga
fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali
ikiwemo ya kutoa maji Ihale, kujenga tanki lenye ujazo wa lita milioni 2 pamoja na mradi wa kuchimba visima virefu.
Katika upande wa sekta ya elimu, amesema “Tumepokea fedha
kiasi cha shilingi bilioni zaidi ya 31,
tumemaliza ujenzi wa sekondari za kata sasa tunaendelea kujenga sekondari za
vijiji nia yetu ni kumpelekea maendeleo kwa wananchi.”
Vilevile, katika afya wilaya hiyo imepokea shilingi
bilioni 10 ambapo wamekarabati na kujenga vituo vipya vya afya.
Aidha, ameshukuru Rais Samia kwa kuendelea kutoa fedha
kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Jimbo lake.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda amepongeza Mhe.
Kiswaga kwa kuandaa mkutano utakaotoa fursa kwa wananchi kuelezwa yale
aliyotekeleza katika kuwaletea maendeleo.
“Kwa miaka mitatu Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais
Samia Suluhu Hassan imeleta shilingi trilioni 5.6 kwa ajili ya utekelezaji wa
miradi ya maendeleo ikiwemo hapa Magu.”
Mhe. Mtanda amesema baada ya Uchaguzi wa Serikali za
Mitaa, CCM Magu imeshinda katika vijiji 78 kati ya 82 na katika vitongoji 508,
imeshinda vitongoji 484 huku akiwataka wananchi kudumisha amani mara baada ya
uchaguzi huo.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Magu, Enos
Kalambo amesema kuwa Rais Samia na Mbunge wao Kiswaga wamefanyakazi kubwa ya
kuwaletea maendeleo katika wilaya hiyo hivyo wananchi waendelee kuwapa
ushirikiano katika kutekeleza majukumu yao.
0 Maoni