Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Dk. Mwigulu Nchemba (Mb),
ameikaribisha Saudi Arabia kuwekeza Tanzania katika fursa mbalimbali zikiwemo
utalii, kilimo, madini, uendelezaji wa miundombinu pamoja na uchumi wa buluu.
Dkt. Nchemba alitoa mwaliko huo alipokutana na kufanya
mazungumzo na Naibu Waziri wa Wizara ya Uchumi na Mipango wa Saudi Arabia, Eng.
Ammar Naqadi, Kando ya Mkutano wa Jukwaa la Biashara na Uwekezaji,
lililoandaliwa na Ubalozi wa Tanzania, kwa kushirikiana na Kituo cha Uwekezaji
Tanzania (TIC) na Shirika la Kuendeleza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA),
lililofanyika hivi karibuni Mjini Riyadh nchini Saudi Arabia.
Alibainisha kuwa Tanzania inaendelea na mradi wa ujenzi
wa reli ya kisasa (SGR) ambapo imeshakamilika kipande kutoka Dar es Salaam hadi
Dodoma na ujenzi unaendelea kwa vipande vinavyoelekea Mwanza na DRC kupitia
Burundi hivyo ni fursa kwa Saudi Arabia kuwekeza katika miundombinu hiyo ambayo
itachochea ukuaji wa bishara kati ya Saudi Arabia, Tanzania na nchi za Afrika
Mashariki.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Uchumi na Mipango wa
Saudi Arabia, Eng. Ammar Naqadi, alisema kuwa Saudi Arabia iko tayari
kushirikiana na Tanzania katika uendelezaji wa miundombinu ya reli ili
kurahisha usafirishaji wa watu, mazao na mizigo ili kuchochochea ukuaji wa
biashara ambapo ushiriki wa sekta binafsi ni muhimu katika kufanikisha biashara
kati ya nchi hizo mbili.
Alisema nchi hiyo iko tayari kushirikiano na Tanzania
katika fursa za kuendeleza sekta ya madini, kilimo, mafuta na gesi, utalii,
uchakataji wa mazo ya bahari miundombinu pamoja na utalii ambapo wataandaa timu
ya wataalamu kwa kushirikiana na Sekta binafsi kutembelea Tanzania kujionea
fursa za uwekezaji katika sekta hizo ili kujiridhisha na mazingira ya fursa za
Tanzania ili kuweza kuwekeza.
Katika kikao hicho Dkt. Nchemba aliambatana na Mawaziri
wenzake wawili, akiwemo Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jafo,
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Mhe. Dkt. Saada Mkuya
Salum pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia, Mhe. Dkt. Moh’d Juma
Abdalla.
0 Maoni