Mtoto mwenye umri wa miaka mitano, mkazi wa Jijini Dar es
Salaam, mwishoni mwa wiki ametolewa pini kwenye mapafu yake kwa kutumia kifaa
maalum chenye kamera kilichopelekwa moja kwa moja hadi ilipo, kuinasa na kisha
kuitoa ambayo amekaa nayo kwa takribani mwezi mmoja.
Wazazi wa mtoto huyo (majina yamehifadhiwa) wanasema mtoto
wao alianza kupata kikohozi na homa za mara kwa mara ndipo walipompeleka
Hospitali kubwa ya binafsi Jijini hapa ambapo walimfanyia baadhi ya vipimo
vilivyoonesha uwepo wa maambukizi kifuani…akalazwa, kesho yake kufanyiwa kipimo
cha X-Ray na kugundua uwepo wa pini ya kubandikia matangazo ambayo walijaribu
kuitoa bila mafanikio na kuwashauri wazazi hao kumpeleka ama Kenya au Afrika ya
Kusini ili kutolewa pini hiyo.
“Kabla ya kufikia uamzi wa kumpeleka Kenya au Afrika ya
Kusini, mme wangu alisema aliona “clip” kwenye vyombo vya habari kuwa Hospitali
ya Taifa Muhimbili hivi karibuni ilifanikiwa kumtoa mtoto Skrubu (Screw)…hivyo
waliomba wapewe Rufaa kuja Muhimbili ambayo tulipewa na kupokelewa vizuri hapo
Emergency ya Muhimbili ambao walimfanyia X-Ray na kuona pini ilipokaa na
kutuambia kuwa mtoto wanamlaza na atafanyiwa procedure ya endoscope kesho
yake,” amesema mama wa mtoto.
Ameeleza kuwa huduma hiyo ya kumtoa pini ilifanyika vizuri na
kwa mafanikio makubwa ambapo mtoto hakohohi tena kama zamani na ni mwenye
furaha.
“Huduma zinazotolewa Hospitali ya Taifa Muhimbili ni sawasawa
na zile tunazofuata katika hospitali kadhaa kwani kuna watoa huduma wenye
weledi, vifaa tiba vya kisasa, mahali pazuri pa kulala, huduma kwa wateja
(customer care) ni nzuri,” amesema mama huyo.
0 Maoni