Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na
Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema Mradi wa EBARR ambao unasimamiwa na
Ofisi ya Makamu wa Rais umekuwa na lengo la kuinua uchumi kwa wananchi
kujipatia kipato nje ya shughuli zao za kila siku ambazo wanafanya.
Ameyasema hayo akikabidhi cherehani 21 kwa vikundi vitatu
ikiwa sehemu ya wanufaika wa Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa
kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR) inayotekelezwa Wilayani Mpwapwa.
Pamoja na ugawaji wa cherehani hizo pia Waziri Dkt. Jafo
alizindua Mradi wa vikundi vitatu vya Ushonaji Kijiji cha Kiegea, Mbugani na
Kijiji cha Kazania ikiwa pamoja na uzinduzi wa Kisima ambacho kinasaidia vijiji
hivyo kupata maji kwa urahisi.
“Rais wa Jamhuri ya Mkuungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu
Hassan alikusudia mradi huu utekelezwe hapa kwa lengo la kuhakikisha unasaidia
na kubadilisha maisha ya watu wa eneo hili na umegharimu zaidi ya Shilingi
bilioni 1.6 ili kutekeleza shughuli mbalimbali.
“Lengo la Rais, Samia ni kuona miradi hii inaendelea na
kunufaisha watu, hivyo muhakikisha miradi hii inasimamiwa vizuri kwa kuwa
unagusa eneo kubwa la maisha ya watu,” alisema Waziri Dkt. Jafo.
Diwani wa Kata ya Ngh’ambi, Richard Matonya alisema awali
kabla ya mradi huo wananchi walikuwa wanakwenda kuchota maji umbali wa zaidi ya
kilometa 10 lakini kwa sasa imesaidia hata kazi za kilimo ambazo wanakijiji hao
wamekuwa wakifanya.
Mratibu wa EBARR kitaifa, Dkt. Makuru Nyarobi alisema lengo
la miradi hii ni kuwasaidia wananchi katika shuguhuli zao hasa katika uchumi
ndio maana imejikita zaida katika utekelezaji wake vijijini.
"Kuna wale wakulima walikuwa wanakwenda mbali kutafuta
maji lakini sahivi imekuwa tofauti, wakulima nao wamefurahia lakini mafundi
cherehani ambao wengi wao ni wakulima wanajipatia kipato kupitia ushonaji,”
alisema Dkt. Nyarobi.
Mradi wa EBARR unatarajiwa kunufaisha zaidi ya kaya 29,000 na
unakadiriwa kuwafikia wanufaika zaidi ya milioni moja (1,000,000) kupitia
utekelezaji wa shughuli za miradi mbalimbali kama vile upatikanaji wa maji kwa
ajili ya matumizi ya nyumbani, kilimo na ufugaji, shughuli mbadala za
kujiongezea kipato; na urejeshaji wa vyanzo vya maji.
0 Maoni