MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Nurdin Babu, ametoa rai kwa
wataalamu wa misitu nchini kutoa elimu kwa wananchi juu ya fursa za misitu
ikiwamo teknolojia ya hewa ukaa huku akimekemea tabia ya baadhi ya wafugaji
kulisha mifugo yao miti inayopandwa na kusisitiza kutomvumilia kwa yeyote
atakayekutwa akifanya hivyo.
Mhe. Babu ametoa rai hiyo leo Machi 19, 2024 Wilayani Same,
Mkoa wa Kilimanjaro wakati akifungua warsha kuhusu masuala ya uhifadhi wa
rasilimali za misitu ikiwa ni sehemu ya matukio kuelekea kwenye maadhimisho ya
Siku ya Misitu Duniani na Siku ya Upandaji Miti Kitaifa inayofanyika Machi 21
wilayani Same, Kilimanjaro.
Amesema misitu imekuwa na manufaa mengi na kuwa fursa zake
zimekuwa zikiongezeka ikiwamo teknolojia ya hewa ukaa na kuwa wananchi wakizitambua
fursa hizo watahamasika katika utunzaji wa misitu kwa ajili ya fursa za
kiuchumi.
“Misitu imekuwa na umuhimu mkubwa sana kwani inachangia
asilimia 3 ya pato la taifa, vifaa vya ujenzi, upatikanaji wa mvua, kuzuia
mmomoyoko wa udongo na makazi ya wanyama, na fursa zake pia zimekuwa
zikiongezeka kila hadi siku, hivyo hatuna budi ya kuhakikisha misitu
inahifadhiwa.”
“Elimu ikitolewe kwa wadau mara kwa mara na wananchi
wakifahamu fursa zinazopatikana katika misitu watashiriki katika uhifadhi,
hivyo wataalamu wa misitu hakikisheni mnaielimisha jamii katika hili.”
Babu amesema Wilaya ya Same ni miongoni mwa wilaya
zilizoathirika na ukataji holela wa miti na kilimo kisichofuata taratibu ya
mazingira hatua ambayo imechangia vifo vya watoto kutokana na maporomoko ya
udongo.
“Same watu wanalima kandokando ya vyanzo vya maji na magema
tumepoteza watoto wengi hasa kutokana na nyumba nyingi kujengwa china ya
magema, barabara zinaharibika na wakulima wengine wanalima mahindi mpaka kwenye
kingo na udongo unakuwa mwepesi na kuporomoka.”
Katika kuirejesha Wilaya ya Same na Mkoa wa Kilimanjaro kwa
ujumla kuwa ya kijani, Mhe. Babu alimuagiza Katibu Tawala Mkoa huo kusimamia
kwa ukaribu kampeni za upandaji miti ili ipandwe ya kutosha.
“Katibu Tawala wa Mkoa, lazima tukubaliane mtu anaruhusiwa
kupanda miti lakini wanapotaka kukata lazima tujue mti uko wapi na unakatwa kwa
shughuli gani.”
Babu amesema pia Serikali ya Mkoa wa Kilimajaro hautavumilia
wafugaji wanaolisha mifugo yao miti ya serikali inayopandwa na kusisitiza
atakayekamatwa akifanya hivyo basi mifugo hiyo itakuwa ni mali ya serikali.
Pia, amewataka maafisa ardhi kuhakikisha ya kutoa vibali vya
ujenzi kwa mtu ambaye amepanda miti isiyopungua mitano na kumtaka Katibu Tawala
wa Mkoa kulisimamia hilo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni alisema
Wilaya ya Same imekuwa ikimuunga mkono Rais Mheshimiwa Rais Dkt. Samia kwa
kuhakikisha wanahifadhi mazingira kwa kupanda miti ili kukabiliana na
mabadiliko ya tabianchi.
Alisema katika kampeni ya kuifanya Same ya Kijani wamepanda
miti kandokando ya barabara kuanzia mwanzo hadi mwisho wa wilaya na mpaka sasa
zaidi ya miti laki tano imeshapandwa katika kampeni ya kuifanya Same kuwa ya
kijani.
Aidha, mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na
Utalii ambae pia ni Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Ufugaji Nyuki, Bw. Daniel
Pancras amesema Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii inajukumu kubwa
la kuhamasisha upandaji miti pamoja na kuelimisha juu ya upandaji miti ili
watanzania wajue namna bora ya kupanda na kutunza miti.
Na. John I. Bera- Same
0 Maoni