Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara Mhe. Esther Nicholas
Matiko amefika Shule ya Sekondari Nyandoto iliyopo Halmashauri ya Mji wa Tarime
na kuzungumza na Walimu na Wanafunzi wa Shule hiyo.
Akizungumza na Walimu wa Shule hiyo, Mhe. Esther Matiko
amepokea changamoto zinazoikabili Shule hiyo ikiwa ni pamoja na ukosefu wa
huduma ya Maji shuleni hapo, ukosefu wa Mabweni kwa Wanafunzi, upungufu wa
vifaa vya kufundishia (Vitabu vya Masomo ya Sanaa), miundombinu mibovu ya barabara
kufika shuleni hapo nk.
Mhe. Esther Matiko ametumia nafasi hiyo kuwapongeza Walimu wa
Shule hiyo kwa kuendelea kufanya kazi kwa Moyo mmoja na bidii licha ya
changamoto kadhaa kuwepo zinazoikabili Shule hiyo. Sambamba na hilo Mhe. Matiko
ameahidi kwenda kuzisema changamoto hizo Bunge la Bajeti linalotarajiwa kuanza
mwezi wa nne Jijini Dodoma.
Akizungumza na Wanafunzi wa Nyandoto Sekondari, Mhe. Matiko
amewahasa Wanafunzi wa Shule hiyo kutumia muda wao vizuri kwa kujisomea na
kuachana na tabia ya kwenda kujishughulisha na shughuli za Machimbo (Mgodi)
yanayopatikana eneo la Kewamamba Jimbo la Tarime Vijijini.
Mhe. Esther Matiko amewahimiza pia Wanafunzi hao
kujishughulisha na michezo kwa kuwapatia Mpira wa Miguu na Mpira wa Pete kwani
michezo imekuwa yenye manufaa makubwa hivi sasa kwa kutoa ajira, kuimarisha
afya na kujenga mahusiano.
Akizungumza kwa niaba ya Walimu, Mkuu wa Shule hiyo Mwl John
Magesa amemshukuru na kumpongeza Mhe. Esther Matiko kwa namna anavyojitoa
kuhakikisha watoto wa Tarime wanafanikiwa kufikia malengo yao kupitia elimu kwa
kuwapa hamasa, husia na kutoa vifaa mbalimbali vya kielimu mashuleni.
Peter Magwi Michael- Mara
0 Maoni