Diamond apatiwa elimu ya urasimishaji biashara BRELA

 

Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bw. Godfrey Nyaisa leo tarehe 7 Machi, 2024 amekutana na kufanya mazungumzo na Mwanamuziki wa kizazi kipya na Mkurugenzi wa Wasafi Media, Bw. Naseeb Abdul maarufu kwa jina la Diamond Platnumz alipotembelea katika Ofisi za BRELA jijini Dar es Salaam.

Bw. Abdul amesema mbali na kuwa mwanamuziki yeye ni mfanyabiashara na mwekezaji ambaye hutengeneza na kuanzisha chapa na kuwainua vijana ili kujipatia kipato hivyo kama mfanyabiashara BRELA ni kama nyumbani.

“Nilipokutana na Bw.Godfrey Nyaisa na kujitambulisha kwangu alinieleza kuwa, BRELA panafaa kuwa  nyumbani kwako kwasababu una chapa tofauti tofauti hivyo patakusaidia katika kusajili kazi zako ili usipoteze haki, maneno hayo yalikuwa na maana kubwa katika maisha yangu na hapo ndipo nilipobadilisha mtazamo na kugundua vijana wengi wanapoteza haki zao,” ameeleza Bw. Abdul.

Ameendelea kusema kuwa, wasanii, wanamichezo, vijana na yeyote mwenye lengo la kufika mbali kimaendeleo hawezi kwenda mbele kama hajarasimisha biashara yake BRELA na ili kuwa rasmi unahitaji kusajili jina la biashara, kusajili kampuni na kufuata taratibu mbalimbali ambazo serikali wameweka kama njia nzuri ambazo zitalinda na kuwezesha kufika mbali.

Aidha, amesisitiza kuwa ni vyema kujitahidi kujirasimisha na kulinda alama ya biashara na huduma pamoja na vumbuzi BRELA ili kulinda ndoto yako kwasababu ukianzisha jambo na likawa kubwa ukigundua kuna mtu anatumia alama yako, kama yeye amewahi ameisajili kisheria anauwezo wa kukupeleka katika vyombo vya sheria. 

“Kwa watu ambao wanatumia brand zetu pasipo kuwa na haki halali naelewa kibinadamu atakuwa anatafuta riziki lakini nawashauri waache na wasinilaumu baadae  kwasababu sheria itafuata mkondo wake hasa kwa kipindi hiki tumeamua kuwa makini zaidi katika biashara,” ameendelea kusisitiza Bw Abdul.

Amehitimisha kwa kusema kuwa sasa amegundua umuhimu wa sajili na amefanikiwa kuchukua hatua ya kulinda haki zake BRELA baada ya kufahamu kwa kina faida zake hivyo kuepuka hasara kubwa ambayo angeipata na kupelekea kupoteza pato la Taifa.

Chapisha Maoni

0 Maoni