Wataalam kutoka Benki ya Dunia wamepongezwa kwa kutoa mafunzo
ya kuwajengea uwezo Maafisa na wataalam wanaotekeleza Mradi wa Kuboresha
Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW) wa
kushughulikia malalamiko (GRM) na maoni yanayolenga utekelezaji wa mradi.
Akifunga Mafunzo ya siku mbili kwa Maafisa hao, Mkaguzi Mkuu
wa Ndani Wizara ya Maliasili na Utalii Bw. Anakretus Mhidze amesema mchango huo
wa Benki ya Dunia kwa njia ya Mafunzo kwa Wataalam hao, ni wathamani kubwa kwa
kuwa unakwenda kuboresha zoezi zima la upokeaji wa malalamiko kupitia mfumo
maalum wa Mradi wa REGROW.
Bw . Mhidze ameongeza kuwa mradi wa REGROW unaendelea kuleta
matokeo chanya na kuwa msaada mkubwa kwa wananchi huku ukitarajiwa kuimarisha
zaidi uhifadhi na Utalii Kusini mwa Tanzania hivyo uwepo wa mafunzo hayo ni
hatua muhimu kupelekea kufikia malengo ya mradi huo.
Aidha, Bw. Mhidze amewaeleza wahitimu wa mafunzo hayo kuwa
Mafunzo waliyopata ni ya muhimu sana kwani yatawasaidia kutekeleza Mfumo wa
kushughulikia malalamiko bila kikwazo na kuhakikisha malalamiko yoyote
yanayotokana na utekelezaji wa shughuli za mradi yanapokelewa na kushughulikiwa
kwa wakati.
"Kupitia mafunzo haya ninyi mmekuwa wahitimu na mabalozi
mnaoweza kuwafundisha wengine utekelezaji wa mfumo huu kwa kushirikiana nao
katika kupokea na kushughulikia malalamiko yanayohusu mradi," alisisitiza
Bw. Mhidze.
Kwa mujibu wa msimamizi wa Mafunzo wa mradi Bw. Loramatu
Meikoki, Mafunzo hayo yameshirikisha Wataalam kutoka Hifadhi za Taifa Tanzania
(TANAPA), Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), Bodi ya Maji ya Mto Rufiji (RBWB), Bodi ya Utalii Tanzania (TTB),
Taasisi ya Utafiti ya Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) na Wizara ya Maliasili na Utalii
(MNRT).
Na. Sixmund Begashe
0 Maoni