Tume ya Madini yaendelea kutatua changamoto sekta ya madini

 

Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba amesema kuwa Tume kwa kushirikiana na Wizara ya Madini imeendelea kutatua changamoto katika sekta ya madini ikiwa ni pamoja na kuwawezesha wachimbaji wadogo wa madini na kupeleka huduma ya umeme ikiwa ni mkakati wa kuhakikisha mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa unaendelea kukua.

Mhandisi Samamba ameyasema hayo leo Februari 13, 2024 kwenye kikao cha Tume ya Madini kilichofanyika jijini Dodoma kilichoshirikisha Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula, Makamishna wa Tume, Wakurugenzi na Mameneja wa Tume chenye lengo la kupokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Tume kwa kipindi cha robo mwaka. 

Amesema kuwa, pia Tume imeendelea kuhamasisha Taasisi za Kifedha kukopesha wachimbaji wadogo wa madini kupitia  mikutano na majukwaa yaliyofanyika katika nyakati tofauti, kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo kuhusu njia salama za uchimbaji wa madini pamoja na uboreshaji wa miundombinu hususan umeme ili uchimbaji wa madini uwe na tija.

Katika hatua nyingine amesema kuwa, Tume imeendelea kufanya kaguzi kwenye migodi mikubwa na midogo ya madini na kutoa elimu kuhusu uchimbaji salama wa madini, kutatua migogoro kwenye shughuli za uchimbaji wa madini na kuvutia uwekezaji katika Sekta ya Madini kupitia makongamano na maonesho yaliyofanyika ndani na nje ya nchi.

Aidha, Mhandisi Samamba amewataka wachimbaji wa madini nchini kuendesha shughuli zao kwa kuzingatia Sheria na kanuni za madini zilizowekwa.

Awali akitoa taarifa ya leseni za madini zilizotolewa katika kipindi cha kuanzia mwezi Oktoba hadi Desemba, 2023, Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi, Profesa Abdulkarim Mruma amesema kuwa kamati ilipokea maombi mapya ya leseni za madini  2,369 yakijumuisha 81 ya leseni za utafutaji wa madini, 18 ya leseni za uchimbaji wa kati na 2,080 ya leseni za uchimbaji mdogo wa madini, 13 ya leseni za uchenjuaji wa madini  na maombi 177 ya leseni za biashara ya madini ambapo baada ya kufanyika kwa uchambuzi, maombi yote yalipitishwa baada ya kukidhi vigezo.

Ameongeza kuwa, katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2023/2024 (Oktoba hadi Desemba, 2023) Tume ilifanya ukaguzi wa migodi na mazingira uliofanyika katika maeneo ambapo shughuli za uchimbaji wa madini zinafanyika hususan katika maeneo ya usalama, afya, mazingira na matumizi salama ya baruti katika migodi mikubwa, ya kati pamoja na midogo.

Ameendelea kusema kuwa katika kipindi husika, ukaguzi ulifanyika kwenye migodi 14,826 ya uchimbaji mdogo wa madini na maghala ya kuhifadhia baruti katika mikoa 30 yote ya kimadini nchini.

Akielezea kuhusu biashara ya madini katika kipindi husika, Profesa Mruma amesema kuwa kupitia masoko ya madini 42 na vituo vya ununuzi wa madini 99 kiasi cha tani 4.52 za madini ya dhahabu, tani 135.71 za madini ya bati, karati 1,811.49 za madini ya almasi, karati 8,260.54 na tani 8.27 za madini ya tanzanite na kiasi cha karati 28,104.58 na tani 21,732.91 za madini mengine ya vito yaliuzwa katika masoko ya madini.

Profesa Mruma amesisitiza kuwa mauzo ya madini hayo yalichangia makusanyo (mrabaha na ada ya ukaguzi) kiasi cha shilingi bilioni 47.48.

Naye Kamishna wa Tume, Janet Lekashingo ameongeza kuwa katika kipindi cha kuanzia Oktoba hadi Desemba, 2023 kamati ya ushirikishwaji wa watanzania katika sekta ya madini ilipokea mipango 217 ya ushirikishwaji wa watanzania katika sekta ya madini ambapo baada ya kufanyiwa uchambuzi, jumla ya mipango 215 ilipitishwa baada ya kukidhi vigezo.

Akielezea mikakati ya kamati kwenye kuongeza ushiriki wa watanzania kwenye shughuli za madini nchini, Lekashingo ameeleza kuwa ni pamoja na kutoa elimu kwa kampuni zinazomiliki leseni za madini na watoa huduma kwenye migodi ya madini, kuandaa majukwaa na warsha mbalimbali kuhusu utekelezaji wa ushirikishwaji wa watanzania katika sekta ya madini sambamba na kushiriki katika maonesho mbalimbali yanayohusu teknolojia ya madini na kutoa elimu kwa washiriki.



Chapisha Maoni

0 Maoni