Katika mwendelezo wa utoaji huduma za kibingwa na ubingwa
bobezi unaotokana na kujenga uwezo wa watalaam wazawa chini ya Serikali ya
Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Hospitali ya Taifa
Muhimbili, leo kwa mara ya kwanza imefanya upasuaji wa kutoa mfupa kwenye ubavu
na kutengeneza kiungio (joint) cha taya la chini na fuvu ili kumtengenezea
mgonjwa taya jipya la kulia lililoathiriwa na uvimbe.
Akizingumza baada ya upasuaji huo, Daktari Bingwa wa
Upasuaji wa Uso na Taya Dkt Arnold Augustino amesema, mgonjwa huyo amefanyiwa
upasuaji wa kuondoa taya lote la kulia lililoathiriwa na uvimbe na hivyo
kumtengenezea taya jipya kwa kuchukua mfupa kutoka kwenye ubavu ambapo mfupa
huo umepandikizwa kwenye kiungio cha taya.
Ameongeza kuwa mifupa mingine imechukuliwa kutoka kwenye
nyonga pande zote mbili ili kuunganishwa na mfupa uliotolewa kwenye ubavu
kuwezesha kutengenezwa kwa taya sawasawa na taya lake la awali na kisha
kuunganishwa na kipandikizi cha chuma maalum kutengeneza sehemu ya taya
iliyoharibika na ugonjwa.
Amesema, mara baada ya upasuaji huu mgonjwa huyo anategemea
kuendelea kula na kutafuna kama kawaida kwani atawekewa meno bandia kwenye
mfupa wa taya aliotengenezewa
Ameongeza kuwa mgonjwa huyo amefanyiwa upasuaji aina tatu tofauti kwa wakati mmoja, wa kutoa kipande cha mfupa kwenye ubavu, wa pili ni kutoa mifupa kwenye nyonga zote mbili na wa tatu ni kuondoa uvimbe ambapo umechukua saa saba umeshirikisha timu watalaam wa MNH madaktari bingwa wa taya na uso (5) wataalamu usingizi na ganzi (2) manesi wa upasuaji (3) na wataalamu wengine waliokuwepo ni pamoja madaktari wanaosomea ubingwa wa kupasua mataya na uso (3).
0 Maoni