Kamati ya Maafa wilayani Mbarali ambayo Mwenyekiti wake ni
Mkuu wa Wilaya ya Mbarali Mhe. Denis Mwila kwa kushirikiana na Diwani wa Kata
ya Luhanga Mhe. Baraka Mamboleo, wametembelea na kukagua maeneo ya Kata ya
Luhanga yaliyoathiriwa na mafuriko ya mvua zilizonyesha kati ya tarehe
30/01/2024 hadi tarehe 03/02/2024 na kusababisha wananchi kuyakimbia makazi yao
kutokana na kuzingirwa na maji.
Ili kuwafikia wahanga hao kwa haraka zaidi, Kamishna wa
Uhifadhi - TANAPA Musa Nassoro Kuji alitoa ndege ya kuzungukia maeneo yote
yaliyoathirika ili kamati ya maafa wilaya ya Mbarali ifanye tathmini ya ukubwa
wa tatizo. Aidha Kamishna huyo pia, aliwaagiza maafisa na askari wake kutoka
Kanda ya Kusini na Hifadhi ya Taifa Ruaha kushirikiana na Kamati hiyo pamoja na
uongozi wa kijiji ili kunusuru hali hiyo.
Akitoa maelezo ya mafuriko hayo, Diwani wa Kata ya Luhanga
Mhe. Mamboleo aliyekuwa ndani ya ndege hiyo huku akionyesha baadhi ya maeneo
yaliyoathirika alisema, "Tathimini iliyofanywa na viongozi wa kijiji na
vitongoji, wamebaini kuwa, vitongoji vya Matono na Iyala vimeathiri zaidi na
mafuriko. Jumla ya nyumba kumi na saba (17) zimesombwa na maji na kusababisha
familia kadhaa kukosa makazi, na familia nyingine zimejiegesha kwa muda katika
shule ya Msingi Iyala huku taratibu nyingine za kiserikali zikiendelea
kufanyika."
Naye, Mwakilishi wa Mratibu wa Maafa Wilaya ya Mbarali,
ambaye ni Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo- Ndg. Ray Salandi alisema, "Kutokana
na makazi mengi kuzingirwa na maji, mazingira hayo sio rafiki kabisa kwa maisha
ya binadamu hususan ikitokea mlipuko wa magonjwa ya kuhara au kipindupindu
wananchi wengi wataathirika zaidi, hivyo nawasihi wananchi hawa waondoke
haraka kuelekea maeneo salama wakati huu
ambapo kivuko cha daraja kilichokuwa kimezama kutokana na wingi wa maji
kimeanza kupitika baada ya maji kupungua.
Kamati ya maafa imewataka wananchi wanaoishi maeneo
yaliyokumbwa na mafuriko kuondoka mara moja ili kupunguza maafa yanayoweza
kutokea wakati huu na baadae. Kwani tunakoelekea ni msimu wa mvua nyingi za
masika.
Zoezi la kuyazungukia maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko lililofanyika jana tarehe 07.02.2024 lilisimamiwa na kuratibiwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbarali akishirikiana na TANAPA.
Na.Jacob Kasiri - Mbarali
0 Maoni