RED EYES: Wanaotumia maji ya chumvi, mkojo wahatarisha macho

 

Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila imetoa elimu kwa wanafunzi wa shule ya msingi Mloganzila kuhusu ugonjwa wa macho kuwa mekundu (Red Eyes) ambao huambukiza kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine.

Akizungumza wakati wa kutoa elimu hiyo mtaalamu wa macho kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili Mloganzila Bw. Martin Jacob amesema zipo sababu mbalimbali zinazoweza kusababisha macho kuwa mekundu ikiwemo Bakteria, Kirusi (Viral Karatoconjuctivits), Mzio (Allergy) au kuumia jicho.

Bw Martin ameongeza kuwa dalili za ugonjwa huo ni pamoja na macho kuvimba, macho kuogopa mwanga, maumivu ya macho na uono wenye ukungu.

Aidha, Bw Martin amewataka wanafuzi hao pindi waonapo dalili hizo wafike hospitali kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na matibabu na kuwashauri kutotumia bila kupata ushauri wa wataalamu wa afya.

“Baadhi ya watu wamekuwa wakitumia dawa pasipo kushauriwa na daktari wa macho, kutumia maji yenye chumvi na wengine kutumia mkojo ili kutibu macho mekundu “Red Eyes” njia hizo sio salama na zinaweza kuharibu macho na huweza kusababisha upofu.”

Aidha, Bw Martin amewashauri wanafunzi kuzingatia usafi wa kunawa mikono kwa maji safi na tiririka, kuepuka kushikana mikono, kuepuka kutumia dawa ya macho isiyo yako na kuepuka kushika macho kwa mikono ili kuzuia virusi kuingia machoni.

Chapisha Maoni

0 Maoni