Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI)
inaendelea kufanya tafiti zaidi juu ya
madhara na matibabu ya ugonjwa wa ngozi wa Twiga ambao matokeo ya awali yameonyesha maeneo
yanayoathirika ya viungio kwenye miguu (magoti) hususan miguu ya mbele, kuna
vimelea vya bakteria, virusi na fangasi.
Akizungumza wakati wa ufuatiliaji wa matibabu ya ugonjwa huo
katika hifadhi ya Taifa Ruaha, Dkt. Julius Keyyu ambaye ni Mkurugenzi wa Utafiti TAWIRI,
amesema ugonjwa wa ngozi wa Twiga uliogundulika katika hifadhi ya Taifa
Ruaha mwaka 2000 ni tofauti na ugonjwa wa ngozi wa Twiga katika nchi
nyingine duniani
"Tumefuatilia ugonjwa huu kwa nchi nyingine duniani na
kubaini upo tofauti na hapa nchini," amebainisha Dkt. Keyyu.
Dkt.Keyyu amesema asilimia 62% ya Twiga waliopo hifadhi ya Taifa
Ruaha wana ugonjwa wa ngozi ambao pia, umeonekana kwa kiwango kidogo katika
hifadhi za Taifa za Tarangire na Serengeti, na tafiti za awali zimeonesha
madhara ya ugonjwa huo ni pamoja na Twiga wenye ugonjwa kutembea kwa kuchechemea, hivyo kushindwa kukimbia
wanapofukuzwa na wanyama wawindao pia hutembea umbali mdogo kwa siku, kwa wiki
na kwa mwezi ukilinganisha na Twiga wasio na ugonjwa.
Dkt. Keyyu amesema kwa sasa TAWIRI inaendelea na ufuatiliaji
wa matibabu ya ugonjwa huo ili kubaini kisababishi asili cha ugonjwa (primary
agent) na kupata matokeo ya kushauri nini kifanyike ili kudhibiti ugonjwa huu
wa ngozi wa Twiga na kuhakikisha mnyama huyu ambaye ni nembo ya taifa anazidi
kuwepo.
Ikumbukwe utafiti wa ugonjwa huu wa ngozi wa twiga unatekelezwa chini ya Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW) uliopo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii na jukumuu la TAWIRI ni kufanya tafiti .
0 Maoni