Madaktari Bingwa wa Upasuaji Mfumo wa Chakula Ini na
Kongosho wa Hospitali ya Taifa Muhimbili wamemfanyia upasuaji mgonjwa mwenye
umri wa miaka 48 na kutoa mawe 62 yaliyokuwa kwenye mfuko wa nyongo ikiwa ni
mara ya kwanza kutoa kiasi hicho cha mawe kwa mgonjwa hospitalini hapa.
Akizungumza kwa niaba ya Jopo lililoshiriki kufanya upasuaji
huo, Daktari Bingwa Bobezi wa Upasuaji Mfumo wa Chakula, Ini na Kongosho, Dkt.
John Bosco Ngendahayo amesema mgonjwa huyo alikuja hospitalini hapo akiwa na
maumivu makali na mwili uliodhoofika baada ya kupewa Rufaa kutoka Mbeya akiwa
na dalili mbalimbali ikiwemo ugonjwa wa manjano, kuwashwa mwili mzima ambao
ulimfanya ajikune mwili kiasi cha kumsababishia vidonda.
“Mgonjwa alikuwa hajui kuwa ana mawe kwenye mfuko wa nyongo
kwakuwa alikuwa na dalili mbalimbali ila baada ya kumfanyia kipimo cha CT-Scan
kilionyesha kuwa mfuko wa nyongo ulikuwa umeathirika kwa sababu mawe yalikuwa
mengi na nyama za tumbo kushikana hivyo tulishauriana na wataalamu kumfanyia
upasuaji ili kutoa mawe uliochukua saa nne,” ameeleza Dkt. Ngendahayo.
Ameeleza sababu zinazosababisha mtu kupata mawe kwenye mfuko
wa nyongo kuwa ni nyongo kupata mgandamizo ndani ya mfuko wa nyongo na
kujiongeza uzito kutokana na madini ya chumvi au mafuta mwilini (rehemu) ambayo
hutengeneza ujiuji na baadaye kuganda na kutengeneza mawe na mawe hayo baadaye
huyeyuka ila kuna mengine ambayo huwa hayayeyuki.
Pia ameongeza kuwa mtu anaweza kuishi na mawe hayo bila
kujua ila baadaye yanaweza kumsababishia kupata maumivu makali tumboni hasa
upande wa kulia chini ya mbavu, kupata manjano, mwili kuwasha kiasi cha kukosa
usingizi, kupata kichefuchefu, kukosa hamu ya kula na dalili nyingine kama
hizo.
Dkt. Ngendahayo ametoa wito kwa jamii kuwa na utamaduni wa kwenda hospitali kufanya uchunguzi wa afya hasa pale wanapohisi kuwa na maumivu kwenye tumbo au wanapopata manjano.
0 Maoni