SAMIA Bond kuanzishwa ili kuwasaidia wakandarasi wazawa- Mchengerwa

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa ameelekeza OR-TAMISEMI na TARURA, kuanzisha mchakato wa upatikanaji wa hati fungani ya miundombinu ya Barabara (TARURA Infrastructure Bond) ambayo itaitwa ‘SAMIA Bond’ kwa kushirikiana na taasisi za kifedha.

Mhe. Mchengerwa ameyasema hayo leo tarehe 24 Januari, 2024 kwenye kikao kazi cha Wizara yake ya Ofisi ya Rais TAMISEMI ,TARURA, Makatibu Tawala Wasaidizi (Miundombinu), Makandarasi Wazawa,Wataalamu Washauri na Taasisi za Kibenki kilichofanyika kwenye ukumbi wa kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Nyerere (JNICC ) Jijini Dar es Salaam.

Waziri Mchengerwa Amesema kwamba lengo la kuanzishwa kwa hati fungani hiyo ni kuwasaidia Makandarasi Wazawa kukabiliana na changamoto za kifedha wanazokupambana nazo na kuwawezesha ili miradi umwanayokuwa wamepewa iweze kukamilika kwa wakati na ufanisi.

“Matarajio yangu ni kuwa, hati fungani hii italeta mapinduzi makubwa kwenye sekta ya miundombinu ya Barabarainayojengwa na TARURA na itaendana na kasi ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwashirikisha na kufanya kazi na sekta binafsi, katika kutatua na kubuni mbinu za kuchochea gurudumu la kuwafikishia maendeleo wananchi,” amesema Mhe. Mchengerwa.

Waziri Mchengerwa amesema kwenye eneo muhimu la matengenezo ya barabara, fedha hupatikana kutokana na makusanyo ya kila mwezi hivyo matengenezo hutegemea kupatikana kwa fedha baada ya makusanyo, na kuongeza kuwa hali hii wakati mwingine husababisha matengenezo kuchelewa.

“Tafiti mbalimbali za Benki ya Dunia zinaonesha kwamba kuna madhara makubwa kiuchumi pale kazi za matengenezo ya barabara zinaposubiri au kuahirishwa na wameonesha kwamba ukiwekeza Dola Moja ya Kimarakeni kwenye matengenezo ya barabara zilizo katika hali nzuri sasa utaokoa Dola Nne hadi Kumi za Kimarekani kulinganisha na iwapo matengenezo hayo yangeahirishwa.”

Hata hivyo amesema ndoto yake ni kuwatengeneza Wakandarasi wazawa mabilionea ambao watafanya kazi bila kushikwa mkono na kuishi ndoto ya kumsaidia Rais Dkt. Samia.

Kikao kazi hicho kwa upande wa TAMISEMI Kimehudhuriwa pia na Naibu  Waziri wa OR TAMISEMI Mhe.Deo Ndejembi,Naibu katibu Mkuu OR TAMISEMI anayeshughulikia Miundombinu Maandisi Rogatus Mativila,Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor Seff pamoja na wawakilishi wengine Mbalimbali wa Wizara na Kamati ya kudumu ya Bunge ya TAMISEMI.

Chapisha Maoni

0 Maoni