RC Makalla atoa maagizo ya kukabiliana na kipindupindu Mwanza

 

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Amos Makalla amewaagiza wataalam wa afya wa wilaya zote katika mkoa huo kuweka mikakati ya kudhibiti na kuhudumia wagonjwa wa kipindupindu kufuatia kuwepo kwa wagonjwa 28 wa ugonjwa wa kipindupindu mkoani humo.

Makalla ametoa wito huo leo Januari 10, 2024 wakati wa kikao chake na wajumbe wa Kamati ya Huduma ya Afya ya Msingi mkoani humo ili kuwekeana mikakati ya kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa huo ulioanzia Wilayani Magu.

"Tuelewane wataalam wa afya, kama leo tuna wagonjwa 28, tukitoka hapa nataka tudhibiti ugonjwa huu usienee mkoani hapa na ili kufanikisha hilo ni lazima tuwe na mikakati ya pamoja ya makusudi ya kudhibiti tatizo hili lisisambae tena kwa ushirikiano mkubwa," amesema  Makalla.

Aidha, Makalla amebainisha kuwa kipindupindu kinatokana na vimelea vya uchafu vitokanavyo na matendo kama chakula kuandaliwa bila kunawa mikono na kupelekea mtu kula uchafu na kama mtaani watu wataendelea kuwa na utamaduni wa mama ntilie kuuza chakula kwenye mazingira yasiyo masafi na kwamba mazingira hayo yatafanya ugonjwa kuendelea kusambaa.

"Nataka miwaambie wananchi kwamba hakuna gharama zozote kwa mgonjwa wa kipindupindu kutibiwa, mtu yeyote mwenye dalili za Ugonjwa wa Kipindupindu afikishwe hospitalini haraka na sio kumhudumia nyumbani au kwa waganga wa kienyeji na serikali tumejipanga kuwahudumia," amesisitiza Makalla.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dr Thomas Rutachunzibwa amebainisha kuwa hadi sasa wilaya zilizoathirika ni tatu za Magu, Nyamagana na Ilemela huku Magu ikiathirika zaidi kwa kuwa na wagonjwa 21  hadi sasa na kwamba tayari kuna vituo vitatu vya kutolea huduma kwa wagonjwa wa kipindupindu.

"Dalili za kipindupindu zinaanza kujitokeza ndani ya masaa 24 hadi 72 baada ya kupata maambukizi na mtu hukosa maji mwilini kutokana na kutapika na kuharisha hivyo jamii lazima iwe na matumizi sahihi ya vyoo, kuosha chakula kama matunda kwa maji ya moto, kutumia maji yaliyochemshwa na kuchunjwa vizuri," ameeleza Dkt. Rutachunzibwa.

Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Huduma ya Afya ya Msingi wa mkoa wa Mwanza wakisikiliza kwa makini maagizo ya Mkuu wa Mkoa Makalla kuhusiana na mikakati ya kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu mkoani huo.


Chapisha Maoni

0 Maoni