Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga amekagua
maendeleo ya Ujenzi wa Miundombinu ya Kupimia Mafuta yanayoingia na kutoka
nchini Pamoja na Ujenzi wa Mapipa mapya ya Kuhifadhi Mafuta Bandarini.
Mhe. Kapinga amefanya ziara hiyo jana tarehe 9, Januari 2024,
ikiwa ni kufuatilia maelekezo ya Mhe. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
aliyoyatoa mwishoni mwa Mwezi Oktoba, 2023 alipotembelea Wakala huo na kuagiza
kuwa Ujenzi wa Miundombinu Mipya ya kupimia Mafuta yanayoingia na kutoka nchini
(Flow Meter) ikamilike kwa wakati na isiathiri utendaji kazi.
Flow Meter inamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100 na
Mapipa hayo mapya yanamilikiwa na Serikali kwa Asilima 50 kupitia Kampuni yake
ya Uhifadhi wa Mafuta TIPER Pamoja na Kampuni ya Orxy kwa Asilima 50 na yana uwezo
wa kuhifadhi Lita za Ujazo Milioni 60.
Mara baada yakuona maendeleo ya Ujenzi huo, Mhe. Kapinga
amesema kuwa Ujenzi wa miundombinu hiyo unaendelea vizuri na utakamilika kwa
wakati kama ilivyoelekezwa.
Amesema kukamilika kwa Ujenzi wa Mapipa hayo mapya
kutaongeza ufanisi wa kuhifadhi mafuta mengi zaidi tofauti na ilivyo sasa na
kwa upande wa Flow Meter kutapunguza foleni za Meli za Mafuta Bandarini.
Baada ya ziara hiyo
Mhe. Kapinga alipata fursa ya kuzungumza na Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala huo
Pamoja na Menejimenti ambapo Pamoja na mambo mengine ameulekeza wakala huo
kueleza Umma majukumu wanayofanya katika kuwa hudumia watanzania.
Sambamba na hilo amewataka PBPA kutumia njia mbalimbali
ikiwemo Vyombo vya Habari, Mikutano pamoja na Semima kwa watu wa makundi
tofauti ili taarifa zao ziwafikie wananchi wote kwa haraka na wakati sahihi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya PBPA, Mhandisi
Lutengano Mwakahesya Pamoja na Mtendaji Mkuu wa PBPA, Erasto Simon wamemueleza
Naibu Waziri huyo kuwa wamepokea maelekezo yote na kuahidi kuyafanyia kazi.
Katika ziara hiyo Naibu Waziri ameambatana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Athumani Mbuttuka, pamoja na Viongozi wengine waandamizi kutoka Wizara ya Nishati na PBPA.
0 Maoni