Muhimbili yaokoa maisha ya mgonjwa aliyeishi miaka 11 na karatasi ya pipi mwilini

 

Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MHN) imefanikiwa kutoa karatasi la pipi kwenye mapafu ya mgonjwa ambaye alikaa na karatasi hiyo mwilini mwake kwa muda wa miaka 11.

Akiongelea tukio hilo Daktari wa Mapafu wa Muhimbili Dkt. Hedwiga Swai amesema karatasi hilo lilikuwa limekaa kwenye njia ya hewa ya mgonjwa huyo mwenye umri wa miaka 53.

Dkt. Swai amesema mgonjwa huyo alibainika kuwa pafu la kushoto limeharibika, limepanuka na linatoa usaha pamoja na kukohoa makohozi yanayonuka.

Ameeleza kwamba mgonjwa huyo alishatibiwa kwa dawa za Kifua Kikuu (TB) wakidhani kuwa na TB pamoja na vipimo vyote kutoonyesha kuwa na TB.

Amesema walibaini kitu ambacho si cha kawaida kwenye mapafu ya mgonjwa huyo baada ya kuingiza mwilini mwake kifaa kinachoita Scope kwenye upande wa kushoto wa pafu lake.

Ameongeza kuwa baada ya kuondoa uvimbe wakaona kitu ambacho si cha kawaida na wakakivuta kwa kupitia puani na kugundua kuwa ni karatasi ya plastiki.

Dk. Swai amesema mgonjwa huyo aliwaambia mwaka 2013, alimeza karatasi inayofungia pipi na alienda hospitali hawakuona tatizo, baada ya hapo aliendelea kukohoa na kutumia dawa bila mafanikio.



Chapisha Maoni

0 Maoni