Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Ustawi na Maendeleo
ya Jamii imeridhishwa na utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili
Dhidi ya Wanawake na Watoto MTAKUWWA wa mwaka 2017/18-2021/22.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Riziki Lulida akizungumza
wakati wa kikao cha kupokea taarifa ya utekelezaji wa Mpango huo kutoka Wizara
ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, jijini Dodoma
Januari 22, 2024 amesema
Wizara hiyo inafanya kazi kubwa hivyo ni jukumu la Kamati
kuhakikisha bajeti ya utekelezaji wa majukumu yake inaongezwa.
Mhe. Riziki ameitaka Wizara kuangalia zaidi wanawake na
watoto wenye ulemavu sambamba na suala zima la mmomonyoko wa maadili
unaochochewa na baadhi ya vipindi kwenye baadhi ya Vyombo vya Habari nchini.
Miongoni mwa wajumbe
wa Kamati hiyo Mhe. Neema Lugangira akichangia mjadala wa taarifa hiyo, ametoa
pongezi kwa Wizara kwa kazi kubwa ya MTAKUWWA iliyowezesha kuongezeka kwa
wananchi kutoa taarifa kutokana na kuwa na imani na Serikali kufanyia kazi.
Mhe. Neema amempongeza pia Waziri Dkt. Dorothy Gwajima kwa
jitihada zake binafsi za kujibu haraka hoja za wananchi hasa upande wa mitandao
ya kijamii na kuzifanyia kazi kwa wakati kisha kuishauri Wizara kushughulikia
ukatili wa kijinsia kwenye Vyuo vya Elimu ya Juu hasa kwa wanafunzi wenye
mahitaji Maalum.
Rugangira ameiomba Wizara kuangalia pia ukatili wa wanawake
na watoto kwenye mitandao ya kijamii,
wanawake wafanyabiashara na wanasiasa kwani wanapitia zaidi ukatili wa
kijinsia.
Naye Mhe. Katani Katani ameishauri Wizara kuandika andiko
mahususi la kuomba fedha kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yake hasa yale ya
kipaumbele, ili kuwezesha Kamati hiyo kujenga hoja ya kuongezwa kwa Bajeti.
Kwa upande wake Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ameishukuru Kamati hiyo
kwa kuelewa ukubwa wa Wizara na majukumu yake kwa mustakabali wa Taifa na
kuwaomba wajumbe wa Kamati hiyo kuendelea kushauri wadau wengine ili mapinduzi
ya uendeshaji yafanyike kama timu moja na kuleta uwajibikaji wa pamoja.
Amesema Kamati hiyo ina ukubwa wa kuweza kuunganisha Kamati
nyingine zote pamoja na Wizara za Kisekta katika kuwekeza kwenye Ajenda ya
Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto kwani ndio waathirika wakubwa
ukatili.
Akiongea wakati wa kikao hicho Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Seif Shekalaghe ameihakikishia Kamati hiyo kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na kuyafanyia kazi ili mpango mpya wa kutokomeza ukatili ufanyike kwa ufanisi.
Na. WMJJWM- Dodoma
0 Maoni