Serikali kupitia Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA)
imesaini mkataba wa makubaliano na Serikali ya China wenye lengo kuendelea na
utekelezaji wa mradi wa Ngorongoro- lengai Geopark.
Mradi huo utakaogharimu Shilingi Bilioni 25 ambazo
zinatolewa na Serikali ya China umesainiwa na Kamishina wa Uhifadhi NCAA
Richard Kiiza na Kaimu balozi wa China Nchini Tanzania kwa ajili ya ujenzi wa
miundombinu ya utalii wa Miamba ( Geopark) ambapo ujenzi huo unatarajiwa
kukamilika mwezi Juni, 2025.
Kamishina Msaidizi mwandamizi wa Uhifadhi anayesimamia
Urithi wa Utamaduni na Jiolojia Mhandisi Joshua Mwankunda amebainisha kuwa
Ujenzi huo utahusisha miundombinu ya makumbusho kubwa na ya kisasa ya jiolojia,
vyoo vya wageni katika kreta ya empakaai
na kwenye nyayo za zamadamu wa kale zilizoko Laetoli.
Aidha ujenzi huo pia utahusisha sehemu za watalii kutazama
na kufurahia sura za nchi (viewing platforms) katika eneo la empakaai, seneto
na oldoinyo Lengai, jengo la kuwezesha utafiti na utalii wa kuona nyayo za zamadamu wa
kale Laetoli, miundombinu ya kutoa tafsiri za rasilimali za utalii za
kijiolojia kwenye maeneo yapatayo 100.
Kamishina Mwankunda ameeleza kuwa miundombinu hii itaongeza
vivutio vya utalii na muda wa watalii kukaa ndani ye Eneo la hifadhi ya
Ngorongoro pamoja na wilaya za Monduli na Karatu mkoani Arusha.
Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi NCAA Bw. Richard Kiiza amepongeza jitihada za mheshimiwa Rais
Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake zilizopelekea kupata msaada huu wa
uendelezaji wa jiopaki ya Ngorongoro- Lengai kutoka nchi ya uchina.
Jiopaki Ngorongoro-
Lengai ndio jiopaki pekee kwa sasa afrika kusini mwa jangwa la sahara na ya
pili baraka afrika.
Utalii wa miamba na sura za nchi ni aina mpya ya utalii unaovutia wageni wengi duniani kwa sasa.
Na. Mwandishi wetu- NCAA
0 Maoni