Meneja wa TARURA Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel
Ndyamukama ameagizwa kuanza mara moja usanifu wa barabara ya Magole
Estate-Mfuru pamoja na ujenzi wa mifereji ya maji katika mji wa Kilosa.
Agizo hilo limetolewa na Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi
Victor Seff wakati wa ukaguzi wa
miundombinu ya barabara na mifereji ya maji iliyoathirika na mvua zinazoendelea
kunyesha wilayani hapa ambapo katika ukaguzi huo aliongozana na Mbunge wa Jimbo
la Kilosa Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi.
Katika Kata ya Kitete walijionea uharibifu wa Barabara ya
Magole Estate-Mfuru yenye urefu wa Km. 4.5
na Kata ya Mbuni walijionea mfereji wa maji unaosababisha mafuriko ya
maji maeneo ya mjini.
Hata hivyo Mhandisi Seff aliwataka wananchi wa mji wa Kilosa
kuunda vikundi vya kijamii kwa ajili ya kufanya kazi za kusafisha barabara na
mifereji ili waweze kutunza miundombinu wanayojengewa na Serikali lakini pia
kuwaongezea vipato na kuondokana na umaskini.
Naye, Diwani wa Kata
ya Mbuni Shabani Maringo ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa ujenzi wa mifereji ya maji katika mji wa
Kilosa ambayo imepunguza madhara ya mafuriko kwa kiasi kikubwa katika mtaa wa
Viwandani,Madaraka, Mjini, Makaburini na Shule ya Msingi Kichangani.
Amesema athari wanazopata sasa zinatokana na maji yaliyoelekezwa kutoka kwenye matoleo ya maji ya mradi wa SGR na kuiomba TARURA kujenga mifereji mingine ili kuyachepusha maji hayo yanayozidi kwenye mfereji wa awali pamoja na kumalizia ujenzi wa mfereji wenye urefu wa mita 750 uliochimbwa kwa nguvu za wananchi.
0 Maoni