Mameneja wa Mikoa na Wilaya wa Wakala ya Barabara Vijijini
na Mijini (TARURA) nchini wametakiwa kufanya kazi kwa weledi katika utekelezaji
wa majukumu yao.
Hayo yamesemwa na Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor
Seff wakati wa kikao cha pamoja cha Menejimenti ya Wakala huo na Mameneja wa
Mikoa na Wilaya kilichofanyika kwenye ukumbi wa JNICC jijini Dar es Salaam.
Mhandisi Seff alisema kufanya kazi kwa weledi itasaidia
kukamilisha majukumu yao kwa wakati na kwa ufanisi na hivyo kuonesha kwamba
wanaweza kwani watakua wamefanya kazi kama inavyotakiwa.
Aidha, Mhandisi Seff amewataka Mameneja hao katika kipindi
hiki cha msimu wa mvua nyingi hususan
inapotokea dharura waweke alama ambazo zitamuonesha mwananchi kwamba eneo
fulani halipitiki na ili kuepusha ajali zinazoweza kujitokeza.
Hata hivyo Mhandisi Seff amewapongeza Mameneja hao kwa kazi
kubwa wanazofanya katika maeneo yao ya kazi kwa kuendelea kuwahudumia wananchi.
Kuhusu maadili ya wafanyakazi wa TARURA , Mkurugenzi wa
huduma Saidizi wa wakala huo Bi Azimina Mbilinyi alitumia kikao hicho
kuwakumbusha viongozi na watumishi wote kwaujumla kuendelea kufanya kazi kwa
weledi kwa kuzingatia misingi na kanuni
za utumishi wa umma kwani zipo wazi na zinafahamika.
0 Maoni