Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila imepokea msaada wa
magari mawili ya kukubea wa wagonjwa (ambulances) kutoka Serikali ya Korea
Kusini kupitia Taasisi yake ya Korea Foundation for International Health Care
(KOFIH) wenye thamani ya takribani TZS. Mil 372.
Akipokea magari hayo kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mkuu wa
Idara ya Matibabu nje ya nchi, Wizara ya Afya Dkt. Asha Mahita ameishukuru
Serikali ya Korea Kusini kwa ushirikiano unaoendelea kutoa katika kuboresha
huduma za afya hapa nchini.
“Kwa niaba ya Serikali ninawashukuru sana kwa msaada huu
kwani mmeunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais
Dkt. Samia Suluhu Hassan ambayo hivi karibuni ilinunua na kusambaza magari ya
kubebea wagonjwa zaidi ya 600. Magari hayo yalisambazwa nchi nzima ikiwa ni
jitihada za kuhakikisha kuwa hakuna Mtanzania anayepoteza maisha anapopata
ajali au ujauzito,” Dkt. Asha.
Dkt. Asha ameongeza kuwa lengo la Serikali ya Awamu ya Sita
ni kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa kitovu cha tiba utalii Afrika Mashari na
Kusini mwa Jangwa la Saraha kwa kutoa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi
zenye ubora wa hali juu katika ukanda huo.
Kwa upande wake, Balozi wa Korea Kusini nchini Tanzania,
Dkt. Kim Sun Pyo ameupongeza uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili -Mloganzila
kwa kuendelea kuimarisha huduma ambazo zimeifanya kuwa tegemeo nchini.
Dkt. Pyo ameongeza kuwa Serikali yake kupitia KOFIH imetoa
msaada huu kwa kutambua kuwa uhai wa watu ni muhimu sana na kubainisha kuwa
magari ya kubebea wagonjwa yana nafasi kubwa katika kuokoa maisha ya mwanadamu.
Naye, Naibu Mkurugenzi Mtendaji MNH-Mloganzila Dkt. Julieth
Magandi amesema magari hayo yametengenezwa mwezi Agosti 2023 hivyo ni ya kisasa
na yana vifaa tiba ambayo ni nadra sana kuvipata katika magari mengine ya kubebea
wagonjwa.
Akitoa shukurani kwa niaba ya wafanyakazi wa MNH -Mloganzila, Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Tiba, Dkt. Faraja Chiwanga amesema magari hayo yamesaidia kutatua changamoto za magari ya kubebea wagonjwa hospitalini hapa ambayo yalikuwa machache na mengine chakavu.
0 Maoni