Diwani aliyemchapa makofi Mwenyekiti wa CCM atiwa mbaroni

 

Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza linamshikilia diwani wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Ilenza wilaya ya Sengerema Mneke Mauna, anayetuhumiwa kumchapa makofi Mwenyekiti wa CCM wa Kata ya Ilenza Lazaro Lubalika.

Inadaiwa tukio hilo la kumchapa makofi Mwenyekiti wa CCM wa kata ya Ilenza limetokea Januari 20, 2024 majira ya tisa mchana baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa kuziba nafasi ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa kata hiyo, kufuatia Mwenyekiti aliyekuwapo kufariki dunia.

Mwenyekiti wa CCM kata ya Ilenza Lazaro Lubalika amesema baada ya kumalizika uchaguzi alienda nyumbani kwa ajili ya kubadilisha nguo ya chama ili aendelee na na shughuli zake nyingine ndipo diwani huyo akamuita na kuanza kumshambulia kwa maneno makali akimtuhumu kuunda genge na kula njama ya kumuwekea sumu kwenye kipaza sauti kwenye mkutano wa mbunge uliofanyika hivi karibuni kijijini hapo.

Kufuatia mzozo huo Diwani Mauna alidaiwa kumchapa makofi Mwenyekiti huyo wa CCM kata ya Ilenza na kumsababishia maumivu, ambapo tukio hilo liliripotiwa katika Kituo Kidogo cha Polisi cha Nyakaliro na kupatiwa RB AKO/URa/24/2024 na polisi kuanza kumsaka mtuhumiwa.

Akizungumza kwa njia ya simu Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza Wilbroad Mutafungwa amethibitisha kushikiliwa kwa diwani huyo wa Kata ya Ilenza wilayani Sengerema Mneke Mauna (CCM) kwa tuhuma za kumushambulia kwa makofi hadharani Mwenyekiti wa CCM Kata ya Ilenza Lazaro Lubalika

"Nikweli tunamshikilia kwa kosa la shambulio la kupinga mkofi hadharani Mwenyekiti wa CCM Kata ya Ilenza Lazaro Lubalika na kumsababusha maumivu, tunaendelea na mahojiano na itakapothibitika atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili,”amesema Kamanda Mutafungwa.

Chapisha Maoni

0 Maoni