Waziri Silaa amsimamisha kazi Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi

 

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa, amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi aliyeandaa Waraka uliochangia kusababisha kadhia ya kuibuka kwa ujenzi wa vituo vya mafuta kwenye makazi ya watu kama uyoga.

Mhe. Silaa ametoa agizo la kumsimamisha kazi mkurugenzi huyo leo Jijini Dar es Salaam, katika mkutano wake na Wahariri na Waandishi wa Habari alioitisha kuelezea mambo aliyoyafanya katika siku 100 akiwa kwenye wizara hiyo, tangu ateuliwe na Rais kushika wadhifa huo mwezi Septemba.

“Waraka wa Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi ndio uliochangia kadhia hii yote ya kuibuka kwa vituo vya mafuta kama uyoga kwenye makazi ya watu, jambo ambalo ni hatari linaweza kusababisha maafa, hivyo natangaza kuanzia leo kumsimamisha kazi mkurugenzi huyo,” alisema Mhe. Silaa.

Amesema kwamba Wizara yake haitowavumilia watendaji wasiotaka kubadilika na kuwatumikia wananchi kwa uadilifu, “Hatuwezi kuwavumilia watumishi wasiotaka kubadilika, watumishi kama hawa hawatofanyakazi katika Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi”.

Katika kuonyesha kwamba hatua kadhaa zimechukuliwa kwa watumishi wa wizara hiyo wasiotaka kubadilika, Waziri Silaa amesema hadi sasa wizara yake imeshawasimamisha kazi maafisa ardhi 13 kwa tuhuma mbalimbali katika mikoa tofauti.

Aidha, Waziri Silaa amepiga marufuku kufanywa kwa mabadiliko ya michoro ya mipango miji pamoja na mabadiliko ya matumizi ya viwanja, na kuongeza kwamba iwapo kutahitajika kufanyika mabadiliko yoyote yataanzia kwanza kwa wananchi wa eneo husika katika vikao vyao.

Pia,  Mhe. Silaa amepiga marufuku Wenyeviti wa Serikali za Mitaa kujihusisha na uuzaji wa ardhi kwa kuwa ni kinyume na sheria na kuwashauri wananchi wanaotaka kununua ardhi wawatumie wataalam wa ardhi kutoka Ofisi za Kata.

Chapisha Maoni

0 Maoni