Wataalam kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wanawake na Makundi Maalum wamewahimiza wadau wanaoendesha Mashirika Yasiyo ya
Kiserikali mkoani Mtwara kuhuisha taarifa sahihi na muhimu juu ya Mashirika yao
katika mfumo wa kidigitali ulioboreshwa (NIS).
Hayo yameelezwa katika mkutano wa majumuisho baina ya Katibu
Tawala Msaidizi Mipango na Uratibu Mkoa wa Mtwara Abdillah Mfinanga, Wataalam
kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii na Wawakilishi wa Mashirika Yasiyo ya
Kiserikali Desemba 21,2023.
Akizungumza katika kikao hicho Katibu Tawala Msaidizi
Abdillah Mfinanga amefafanua kwamba ulipaji wa ada peke yake hautoshi
kulitambulisha Shirika kuwa hai na kuna ulazima wa kila Shirika kujaza taarifa
zinazotakiwa ili kurahisha ufuatiliaji wa Shirika na kazi wanazofanya.
“Tumekadiriwa kuwa na asilimia 50 katika zoezi zima la
ujazaji wa taarifa na hiki si kitu kizuri, natumaini tutabadilika na kuhuisha
taarifa zinazoendana na mfumo ulioboreshwa (NIS) ili kurahisisha uratibu wa
Mashirika yenu kwa Serikali na utambulishwaji wa huduma zenu kwa wanufaika
lakini pia ufatiliaji wa taarifa kutoka kwa wafadhili” amesema Mfinanga.
Aidha Mtaalam kutoka Ofisi ya Msajili wa Mashirika Yasiyo ya
Kiserikali Charles Mpaka ameyahimiza Mashirika hayo juu ya umuhimu wa
ushirikiano baina yao ili kukua na kustawi.
“Mashirika makubwa yanaweza kuyasaidia Mashirika machanga
kukua kwa kuyashika mkono katika vitu vingi ikiwemo kuwaelekeza namna mzuri za
uandishi wa Miradi, kuwasaidia na vitendea kazi pamoja na hata ushauri wa namna
ya kuendesha miradi yao bila kusahau kuwaelekeza fursa zilipo” amesema Mpaka.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la PAWASO ambae ni
mjumbe wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NACONGO) Mkoa wa
Mtwara Baltazal Komba ameishukuru Serikali kwa jitihada zake katika kuimarisha
mfumo mzima wa utoaji wa huduma kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali tofauti na
awali.
Vilevile Mratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Mkoa wa Mtwara Tabitha Kirangi amesema zoezi hilo la ukaguzi wa Mashirika hayo umemrahisishia kuelewa vizuri changamoto zinazokabili Mashirika hayo na kuahidi kutoa ushirikiano wa karibu zaidi katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto hizo.
Na WMJJWM- Mtwara
0 Maoni