Serikali yaunganisha mashirika ya umma 16 na kuyafuta manne

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo ametangaza uamuzi wa Serikali wa kuyaunganisha mashirika ya umma 16 pamoja na kuyafuta mashirika ya umma manne.

Akiongea leo Prof. Mkumbo amesema kwamba kutokana na mapendekezo ya timu ya wataalamu, Serikali imeridhia kuelekeza kuunganishwa kwa mashirika na taasisi za 16 na kufuta mashirika na taasisi za umma nne.

Ametaja mashirika na taasisi za umma zilizounganishwa kuwa ni Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) yanayounganishwa na kuwa taasisi moja ya utambuzi wa matukio muhimu maishani.

Amesema pia, Benki ya Kilimo Tanzania (TADB) na Mfuko wa Pembejeo za Kilimo (AGITF) zinaunganishwa ili kuwa na taasisi moja itakayohusika na mikipo na ugharamiaji wa maendeleo ya kilimo nchini.

Aidha, Bodi ya Chai inaunganishwa na Wakala wa Maendeleo ya Wakulima Wadogo wa Chai Tanzania (TSHDA), huku bodi ya Nyama nayo inaunganishwa na Bodi ya Maziwa ili kuunda taasisi moja ya kuendeleza na kusimamia mazao ya mifugo yakiwamo ya nyama na nyama na maziwa.

Prof. Mkumbo amesema Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kinaunganishwa na Mamlaka ya Uzalishaji wa Mauzo ya Nje (EPZA) ili kuunda taasisi moja itakayoratibu uwekezaji wa sekta binafsi wa ndani na kutoka nje.

Vilevile Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini (CARMARTEC), Taasisi ya Uhandisi na Usanifu Mitambo Tanzania (TEMDO) na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) zinaunganishwa na kuunda taasisi moja.

Taasisi ya Utafiti wa Chai Tanzania (TRIT), Taasisi ya Utafiti wa Tumbaku Tanzania (TORITA) na Taasisi ya Utafiti wa Kahawa (TACRI) zinaunganishwa na kuwa sehemu ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI).

Prof. Mkumbo ameyataja Mashirika na Taasisi za Umma zinazofutwa au kuvunjwa ni pamoja na Shirika la Uzalishaji la Jeshi la Polisi (TPFCS), Taasisi ya Chakula Lishe (TFNC), Shirika la Elimu Kibaha (KEC) pamoja na Bodi ya Pareto.

Chapisha Maoni

0 Maoni