Serikali imesema kuwa hakuna mwananchi yeyote anayefukuzwa
katika eneo la Loliondo lenye ukubwa wa
kilomita za mraba 2,500 ambalo lilimegwa kutoka pori la akiba Pololeti katika
Wilaya ya Ngorongoro ambalo Serikali ililitoa
kwa ajili ya shughuli za wananchi.
Akizungumza na waandishi wa Habari jijini Dodoma
Msemaji Mkuu wa serikali na Mkurugenzi
wa Idara ya Habari-Maelezo Bw.Mobhare Matinyi
amesema taarifa hizo hazina
ukweli wowote, kwani Serikali ilikabidhi eneo hilo kwa ajili ya matumizi ya
Wananchi kufuatia kumegwa kwa lililokuwa
pori tengefu la Loliondo mwaka 2022.
Amebainisha kuwa awali pori hilo lilikuwa na ukubwa wa kilomita za mraba 4,000 ambapo baada ya kugawanywa
Kilomita za mraba 1,500 ambazo ndio Pori la akiba pololeti zilibaki kwa ajili ya shughuli za uhifadhi na
Kilomita za Mraba 2,500 Serikali ilizitoa kwa ajili ya Wananchi kufanya
shughuli zao za maendeleo.
Bw. Matinyi alisisitiza kuwa
serikali itaendelea kusimamia shughuli za uhifadhi katika eneo la
Ngorongoro na kuwataka wananchi kupuuza taarifa hizo kwa kuwa Serikali inatekeleza majukumu yake
kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na kufuata misingi ya haki za binadamu.
Amewataka wananchi wote wanaoishi katika eneo walilopewa na Serikali lenye kilomita za mraba 2500 kuendelea na shughuli zao na kupuuza taarifa hizo zenye lengo la kupotosha umma.
Aidha, amesema Serikali itaendelea kuheshimu haki za
binadamu katika zoezi la kuhamisha watu wanaojiandikisha kuhama kwa hiyari
kutoka eneo la hifadhi ya Ngorongoro kwenda maeneo mengine nchini.
Matinyi amesisitiza msimamo wa Serikali kuwa inawahamisha wananchi wanaojiandikisha wenyewe kuhama katika eneo la hifadhi ya Ngorongoro na kwamba hakuna ukiukwaji wowote wa haki za binadamu unaofanyika katika utekelezaji wa zoezi hilo.
Ameeleza kuwa serikali ya Tanzania inatekeleza mpango huo
ikiamini katika kutimiza malengo ya dunia ya milenia ya kuhakikisha usalama wa
watu wake, huduma bora za kijamii ikiwemo elimu, afya na maji huku akisema
kwamba serikali itaendelea kuhamasisha wananchi hao kukubali kuhama kwa hiyari.
Bw. Matinyi ameeleza kuwa mtu yoyote au kundi linalotaka
kutembelea eneo la hifadhi ya Ngorongoro wanakaribishwa na wanachotakiwa
kufanya ni kufuata taratibu ili waweze kuruhusiwa kwa kuwa Serikali haina
sababu ya kumzuia mtu yeyote kufika eneo hilo.
Akizungumza hoja ya kuwepo kwa watu asili nchini Tanzania Bw. Matinyi amesema kuwa watanzania wote wanatambulika kwa utaifa wao ambapo kuna zaidi ya makabila 120 na hivyo suala la kuhamisha watu katika hifadhi hiyo lisitazamwae katika kuhamisha kabila fulani bali wananchi wote waliopo huko wanahamisishwa kuhama kadri wanavyojiandikisha.
0 Maoni